Naibu Waziri Kigahe awakaribisha wananchi maonesho ya SIDO Kanda ya Kaskazini, BRELA kutoa huduma papo kwa papo

Na Christina Njovu

Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amewataka wananchi na wajasiriamali katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kutembelea katika mabanda ya washiriki wa maonesho ya SIDO Kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika Viwanja vya Kwaraa mjini Babati ili kupata huduma zinazotolewa na washiriki wa maonesho hayo ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Fredrick Sumaye akisaini katika kitabu cha wageni katika banda la BRELA katika maonesho ya SIDO yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa, vilivyopo Mjini Babati, maonesho hayo yameanza jana tarehe 27 Mei na yatamalizika tarehe 31 Mei, 2021.Karibuni tuwahudumie. (Picha na Christina Njovu).

Mhe. Kigahe amesema hayo alipokuwa akifungua maonesho ya SIDO Kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa vilivyopo Mjini Babati mkoani Manyara.
 
Wakati akitembelea mabanda ya washiriki wa maonesho hayo, ameweza kuzungumza na baadhi ya wajasiriamali ambao wamemuomba kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo na kusaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma ambazo wanazihitaji zikiwemo kusajili wa biashara zao, kupata nembo za ubora na pia kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.

“Tembeleeni maonesho haya ili muweze kujifunza na kufahamu umuhimu wa kusajili Majina ya biashara na Makampuni pia mtaweza kusajili Majina ya Biashara na Makampuni yenu hapa hapa uwanjani katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambao nao ni miongoni mwa washiriki katika maonesho haya. Pia mtaweza kujua mbinu za kutafuta masoko ya bidhaa, fursa za masoko zilizo wazi nchini na mikakati ya kushiriki maonesho mbalimbali yanayoandaliwa na SIDO, lakini na mashirika mengine,” amesema Mhe. Kigahe.
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), akipata maelezo mafupi kutoka kwa Afisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw.Gabriel Girangay (katikati), kuhusu ushiriki wa BRELA katika maonesho ya SIDO Kanda ya Kaskazini, yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa, vilivyopo mjini Babati Mkoani Manyara. Maonesho haya yameanza tarehe 27 Mei hadi tarehe 31 Mei, 2021, karibu tukuhudumie.

Aidha, ameongeza kuwa, wajasiriamali wakiweza kupata mafunzo hayo hivi sasa yatawawezesha kupata ushiriki wa kimkakati kwa kuwa yatawawezesha kushiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa kuwa suala la kufanya biashara ni endelevu linahitaji elimu kila wakati na kuwasishi wafunguke na waendelee kutafuta elimu hususani kutoka shirika la viwanda vidogo SIDO ili biashara zao zizidi kukua.

Awali Mhe. Naibu waziri Kigahe alitembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambalo ni miongoni mwa mabanda ya washiriki katika maonesho hayo alipata maelezo juu ya sababu ya ushiriki wa wakala katika maonesho hayo kutoka kwa Afisa Usajili wa Wakala wa Biashara na Leseni (BRELA) Gabriel Girangay ambaye amemueleza Naibu Waziri Mh.Exaud Kigahe kuwa;

“BRELA imeshiriki katika maonesho ya SIDO kanda ya Kaskazini ili kusogeza huduma zetu karibu , huduma zetu zinatolewa kwa njia ya mtandao huduma hizo ni pamoja na Usajili wa Makampuni, Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma,”amesema.

Afisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw.Gabriel Girangay aliongeza kuwa; Vile vile tunatoa Hataza ambayo ni hati miliki Ubunifu, Utoaji wa Leseni za Biashara kundi A, Utoaji wa Leseni za Viwanda”. Ushiriki huu unatoa fursa kwa Wananchi wa Mkoa wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga wanaohitaji kupata sajili mbali mbali ama waliokuwa wakipata changamoto za kufanya sajili kwa njia ya mtandao kuweza kupata huduma moja kwa moja.

Maonesho haya yaliyoanza jana tarehe 27 Mei yanatarajiwa kufungwa tarehe 31 Mei ,2021, yanawakutanisha wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga BRELA inawakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake ili waweze kuhudumiwa, BRELA tunaipa utu wa kisheria biashara yako.

Post a Comment

0 Comments