Rais Samia akemea wenye mioyo ya choyo, maono mafupi

Katika hotuba yake hiyo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, wale wanaoamini kuwa nchi mojawapo kati ya Tanzania na Kenya inaweza kuendelea kwa kumuangusha mwenzake hilo linawezekana kwa watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Mabunge Mawili ya Kenya (Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate la Kenya kwa pamoja Jijini Nairobi leo tarehe 05, Mei, 2021. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo wakati akihutubia Mabunge Mawili ya Kenya likiwemo Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate la Kenya kwa pamoja jijini Nairobi leo Mei 5, 2021.

Aidha, anakuwa Rais wa pili kutoka Tanzania kuhutubia Bunge hilo, akitanguliwa na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambapo amesema binafsi anashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni washindani, na hivyo uhusiano wa nchi hizo mbili uwe wa kuasimiana na kukamiana.

"Nawashangaa, Kwani Kenya peke yake, wala Tanzania peke yake haiwezi kuendelea peke yake, mbaya zaidi ni kule kuamini kwamba hilo linawezekana tu, mmoja wetu akimuangusha mwenzake.Hilo linawezekana kwa watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu,"amesisitiza.

Amesema, ni bahati mbaya watu hao wapo pande zote mbili za nchi hizo na inatokea mara chache sana wanakuwa ni watumishi wa Serikali na hata wanasiasa wa pande hizo mbili.

"Bahati mbaya sana sio wengi, kwangu mimi na katika awamu yangu ya uongozi nitahakikisha Kenya inabaki ndugu, jirani na mshirika wa mkakati na mbia,"amesema.

Pia amesema, Kenya ni nchi ya tano duniani na ya kwanza kwa Afrika kwa uwekezaji Tanzania ikiwa inatekeleza miradi 513 iliyotoa ajira kwa 51,000.

Rais Samia alisema kutokana na uhusiano mzuri wa nchi hizo, kampuni za Tanzania zimewekeza Kenya, lakini kwa uchache sana, kampuni kama 25 hadi 30 zimesajiliwa na kituo cha uwekezaji cha Kenya zikiwa zimetoa ajira 2000.

Amefafanua kwamba pamoja na pengo hilo la uwekezaji kati ya nchi hizo, bado wanawaalika Wakenya kuja kuwekeza nchini, kwa sababu Tanzania ina mambo mengi, ina rasilimali za kutosha, madini, ardhi, na kinachokosa ni mtaji.

"Kenya mna mtaji wa kutosha karibuni Tanzania,"amesema na kuongeza kwamba dhamira yake ya kwenda Kenya ni pamoja na kuangalia ni kwa namna gani Watanzania watafanya vizuri zaidi kwenye uwekezaji.

Mbali na uwekezaji, Rais Samia alisema ushirikiano wa nchi hizo katika sekta ya biashara nao ni mkubwa na umeendelea kushamiri siku hadi siku, huku akitoa mfano kwamba usafirishaji wa bidhaa za Tanzania kwenda Kenya umeendelea kuongezeka.

Hata kwa Kenya amesema, usafirishaji wa bidhaa umeongeza kiwango cha kuuza bidhaa zake nchi Tanzania kimetoka sh. bilioni 420 hadi 521 mwaka 2020.

Rais amesema hiyo inawasuta viongozi na wanasiasa na inaonesha wananchi wa nchi hizo wapo mbele yao, wanafanya biashara zao kwa ubunifu, lakini wao (viongozi) wanag'ang'ana na sheria na vikwazo na wanawavuta nyuma kidogo.

Rais Samia alisema ni wakati sasa wa viongozi kubadilika na kuwa daraja la kuunganisha watu na sio kuwa vikwazo. Alifafanua kwamba yeye na Rais Uhuru Kenyatta wamekubaliana kuweka utaratibu madhubuti wa kuondoa pilikapilika zinazotokea mipakani zinazotokea wakati wa kuvusha biashara kwenda kwenye nchi hizo.

Ametaja eneo lingine ambalo nchi hizo zinatakiwa kushirikiana ni sekta ya utalii, kwani ikolojia ya nchi hizo mbili zinaingiliana sana.

Aidha, amesema hata vivutio vya utalii navyo vinaingiliana, hivyo wana nafasi ya kuneemeka pamoja kama watashirikiana katika sekta hiyo badala ya kushindana.

Amesema badala ya kunyang'anyana idadi ya watalii, busara inawataka kuwahamasisha waongeze idadi ya siku ambazo watazitumia nchini Kenya na Tanzania na kwa kufanya hivyo, wote tutafaidika.

Mhesshimiwa Samia Amesema mashirikiano hayo yanashamirishwa na hatua kubwa wanazozichukua katika kupambana na ujangili, uhalifu, ugaidi, dawa ya kulevya na uharamia.

"Wahalifu wa Tanzania na Kenya wana ushirikiano mzuri, vyombo vya ulinzi na usalama navyo vishikamane ili kuweza kulinda maeneo hayo ili kushinda ushirikiano wa wahalifu," alisema..

Alisema katika ziara yake hiyo wamekuwa na mazungumzo mazuri ya kuamsha ushirikiano wa nchi hizo mbili, hivyo ana wasiwasi tusije tukawabakiza nyuma.

Amesema awali walikuwa na mazungumzo na Rais Kenyatta yenye kuamsha matumaini makubwa sana ya ushirikiano katika ya nchi hizo mbili.

Pia amesema, hakukuwa na ugumu wala ukakasi wowote katika kufikia muafaka wa mambo waliyokuwa wakijadiliana, wamezungumza kindugu sana.

Rais Samia alisema kilichojitokeza sana katika mazungumzo hayo ni namna nchi hizo mbili zinakubaliana katika mambo mengi, kuliko yale machache wanayotofautiana.

"Hata hayo machache tunayotofautiana yenyewe hayakuwa na misingi imara ya tofauti, bali ni mitazamo tu ya watu, ambapo mitazamo mingi inayoleta ukakasi inachangiwa na kukosekana kwa mawasiliano baini ya nchi hizo," alisema.

Amesema ili kuondoa mitazamo hasa kati ya nchi hizo wamekubaliana kujenga na kuendeleza utamaduni wa kukutana mara kwa mara katika ngazi mbalimbali.

Wakati huo huo, Rais amesema umbali ujenga mashaka na ukaribu uondoa mashaka hayo.
Alisema uamuzi wake kwenda Kenya kwa mara ya kwanza, sio bahati mbaya, bali ni wa makusudi.

Amesema, busara zinaelekeza kwamba ukiwa mpangaji mpya, lazima ujitambulishe kwa majirani, hivyo na yeye kwa nafasi hizo ni mpangaji akaona ajitambulisha kwa majirani na jirani wa kwanza ni Kenya.Tazama hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia mabunge ya Kenya hapa.

Pia amesema, alianza ziara yake Kenya sio kwa sababu ni karibu kijiongrafia, bali ni kwa umuhimu na nafasi ya Kenya kwa Tanzania na uhusiano wa nchi hizo ni wa kipekee sana, ni uhusiano uliofungwa katika mafundo matatu.

Ametaja fundo la kwanza kwamba ni undugu wa damu kati ya wananchi wa nchi hizo, ambao hauzi kutengenishwa na mipaka ya kwenye ramani.

Rais ametaja fundo la pili kuwa ni historia na kwamba kabla ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, nchi hizo tayari zilikuwa zimeanzisha ushirikiano wake zikiwa chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza, huduma zote muhimu, chumi zetu zilifumwa pamoja kabla ya Uhuru.

Kwa mujibu wa Rais Samia, fundo la tatu ni jiografia, kwamba Mungu amejalia hicho kuwa pamoja hata kwenye ikolojia, kwani hata wanyama wa nchi hizo ni majirani, akitolea mfano wanyama aina ya nyumbu akisema wanakwenda kupata mimba Kenya, wanazalia Tanzania.

"Sasa ingekuwa wanyama wana uraia wangekuwa raia wa wapi? Wakitoka Serengeti wanaingia Masai Mara. Lakini hata Tausi wetu waliopo Tanzania wana ndugu zao Nairobi, sasa kama Tausi na wanyama wana undugu, sisi wanadamu tunatengana wapi?" Alihohi Rais Samia huku akiongeza kuwa kutokana ukweli huo, ushirikiano baina ya nchi hizo sio wa hiari, bali ni wa lazima na pande zote zinategemeana kwa kila hali.Rais Samia, Uhuru Kenyatta wasema na wafanyabiashara soma hapa.

Post a Comment

0 Comments