Wafanyabiashara sasa mshindwe ninyi; Rais Samia, Uhuru Kenyatta waeleza; Rostarm Aziz afunguka

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya wamewahakikishia wafanyabiashara wa nchi hizo kuwa Serikali zote mbili zipo tayari kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji katika kukuza biashara na uwekezaji, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.

Viongozi hao wa mataifa hayo ya Jumuiya ya Mashariki kwa nyakati tofauti wameyasema hayo wakati wanahutubia jukwaa la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya jijini Nairobi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na mwenyeji wake Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta wakati nyimbo za Mataifa Mawili ya Tanzania na Kenya wakati zikipigwa mara baada ya kuwasili Ukumbini kwa ajili ya kuhutubia Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania lililofanyika jijini Nairobi.

Rais Samia amesema, "Sasa mshindwe ninyi" ambapo viongozi hao wamewahakikishia kuwa Serikali za nchi zote mbili zipo tayari kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji katika kukuza biashara na uwekezaji katika nchi hizo.

Rais Samia amesema, pamoja na kufungua milango ya biashara na uwekezaji kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege na meli na kwamba juhudi kama hizo zinaendelea.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania lililofanyika jijini Nairobi, Kenya.

Pia ameongeza kuwa, Tanzania imeandaa mpango wa uboreshaji wa mazingira ya biashara (Blue Print) na inarekebisha masuala mbalimbali yakiwemo ya kikodi na kuondoa vikwazo ili wafanyabiashara wa Kenya na mahali pengine wawe huru kufanya biashara na kuwekeza katika uzalishaji utakaosaidia kuzalisha ajira kwa wananchi na kuinua ustawi wao.

Rais Samia ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili wafanyabiashara wengi zaidi wa Tanzania wajitokeze kuwekeza nchini Kenya kama ambavyo wafanyabiashara wa Kenya walivyowekeza kwa kiasi kikubwa nchi Tanzania.

“Tanzania ipo tayari kupokea uwekezaji kutoka Kenya, milango yetu ipo wazi na mikono yetu ipo tayari kuwapokea, Serikali ipo tayari kuwa daraja la kuwezesha biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu, mna bahati kwamba nchi zetu mbili upande mmoja kuna uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna suluhu ya kuondoa vikwazo vya biashara kwa hiyo sasa mshindwe ninyi,”amesema Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya katika Kongamano hilo la Wafanyabiashara lililofanyika jijini Nairobi. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipongezwa na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta mara baada ya kuhutubia katika Jukwaa hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi nchini Kenya. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta mara baada ya kuhutubia katika Jukwaa hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Naye Mheshimiwa Rais Kenyatta amesisitiza kuwa Tanzania na Kenya hazipaswi kushindana katika biashara, bali kushirikiana kukuza zaidi biashara na uwekezaji kati yake ili kuzalisha ajira, kupata fedha za kutoa huduma za kijamii na kukuza ustawi wa wananchi.

Mheshimiwa Kenyatta amewaruhusu wafanyabiashara wa Tanzania kuingia nchini Kenya na kuwekeza bila sharti la kuwa na viza ya biashara na amewaagiza mawaziri wanaohusika kukutana ili kutatua kero zinazokwamisha ufanyaji wa biashara.
Sehemu ya viongozi mbalimbali pamoja na Wafanyabiashara waliohudhuria Kongamano hilo jijini Nairobi. (Picha zote na Ikulu).

Rais Kenyatta alitoa wiki mbili kwa Mawaziri wake kutatua vikwazo vilivyosababisha msululu wa magari katika mipaka ya Holili na Taveta na kumaliza mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa mahindi ya kutoka Tanzania kwenda nchini Kenya, na ametaka kuwepo kwa utaratibu utakaoruhusu vibali vinavyotolewa kwenye kila nchi kukubalika katika nchi nyingine.

Wafanyabiashara wanaokutana katika jukwaa hilo wamewahakikishia waheshimiwa Marais kuwa wapo tayari kuongeza ushirikiano baini yao, kukuza biashara na uwekezaji hasa uzalishaji wa bidhaa kupitia viwanda vya ndani ili kuzalisha ajira na kodi kwa Serikali badala ya kuwa waagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje.

Kauli mbiu ya jukwaa hilo ni “kuboresha biashara, utalii na uwekezaji kati ya Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Afrika Mashariki kwa kutilia mkazo umoja wa forodha”.
Wakati huo huo mfanyabiashara Rostam Aziz akizungumza kwenye kongamano hilo amesema mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na Kenya yanatofautiana, kwani ni rahisi kuwekeza katika nchi moja na ngumu kwa nchi nyingine.

Mfanyabiashara huyo maarufu ameshauri suala hilo kama halitafanyiwa kazi litagharimu uhusiano wa nchi hizo mbili, ushauri ambao ameutoa katika hilo la wafanyabiashara na marais.Kwa matukio mapya endelea hapa.

Rostarm Aziz amesema ni rahisi sana kwa Kenya kuja Tanzania kuwekeza, lakini hali ni tofauti kwa upande wa pili na kwamba ipo mifano ni mingi.

"Kuna kampuni 530 za Kenya ambazo zimewekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.7 nchini Tanzania, lakini kuna kampuni 30 tu za Tanzania zilizofanikiwa kuwekeza nchini Kenya kwa uwekezaji wa Dola milioni 50,"amesema Rostam.

Aidha, kwa mujibu wa Rostam uhusiano huu si ule wa kujenga uchumi kati ya mataifa hayo na kwamba iwapo watashindwa kuufanyia kazi, hawataweza kufanikiwa kutimiza malengo yao.Tazama live kilichojiri hapa.

Akitoa ushuhuda wa hilo, Rostam amesema mwaka 2017 alikwenda Kenya na kufanya mazungumzo na Kenyatta aliyemtaka awekeze nchini humo, lakini hadi sasa suala hilo halijafanyiwa kazi.

“Rais Kenyatta aliniomba niwekeze nchini Kenya na aliniuliza kwamba ningependa kuwekeza kwenye nini, nikamwambia naona kuna fursa kwa upande wa gesi, sasa imepita miaka mitatu bado sijapata majibu kuhusu uwekezaji niliotaka kufanya ambao ungegharimu Dola za Marekani milioni 130,"amesema.

Post a Comment

0 Comments