SERIKALI KUTOA ELIMU YA KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI KWA WANANCHI

Na John Bera-WMU (Same).

Naibu Waziri wa Malialisi na Utalii Mhe. Mary Masanja amesema Serikali imeanza kutoa elimu kwa Wananchi namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kupitia Wataalamu wa masuala ya Wanyamapori ikiwa lengo ni kulinda usalama wa Wananchi na mali zao.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Wakazi wa Kijiji cha Maore kilichopo katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ambapo amewahakikishia Wananchi hao kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inatatua kero ya Tembo kuingia kwenye maeneo ya makazi yao.

Naibu Waziri Mhe.Masanja ametoa kauli hiyo leo katika kijiji cha Maore kilichopo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro wakati akizungumza na wakazi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakikumbwa na uvamizi wa Tembo katika maeneo yao.

’’Serikali inasikitika inapoona Wananchi wake wanateseka na wanyamapori wakali kama vile tembo, Tumetafuta mbinu mbadala ya kuhakikisha Wananchi mnafundishwa namna bora ya kukabiliana na Wanyamapori hawa,"amesisitiza Mhe. Masanja.

Amesema, mbali ya kutolewa kwa elimu hiyo ya kukabiliana na Wanyamapori hao, Serikali itagawa vifaa maalum kwa ajili ya kuwafukuza tembo wanapofika katika maeneo yao ikiwa pamoja na kuwapatia namba ya simu za askari watakaokuwa wakipatiwa taarifa pale tembo wanapovamia maeneo yao ili waje kutoa msaada kwa haraka kabla tembo hawajasababisha madhara kwa Wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mary amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Kushirikiana na Wizara ya Ardhi itatenga maeneo maalumu kwa ajili ya Mifugo ili kuepusha wananchi kukumbwa na changamoto ya kuharibiwa mali zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news