Simba SC yatafuna viporo hatua kwa hatua, Morrison awakera Namungo FC

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Simba SC wameiadhibu Namungo FC mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa ni hatua ya kukamilisha viporo vyake.Mtanage huo wa Mei 29, 2021 ulipigwa katika dimba la Majaliwa lililopo mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Awali, Namungo ilitangulia kwa bao la Mrundi, Nzigamasabo Steve dakika ya 22, kabla ya Simba kuzinduka kipindi cha pili kwa mabao ya washambuliaji, Mkongo Chris Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 79, John Raphael Bocco dakika ya 84 na kiungo Mghana, Bernard Morrison dakika ya 88.

Katika mtanange huo, winga wa Kimataifa wa Ghana anayesakata kabumbu nchini Tanzania katika klabu ya Simba, Bernard Morrison goli lake lilitajwa kuwa la aina yake.

Ni baada ya kugonga ncha kali akiwa nje ya 18 kwa shuti lililomshinda mlinda mlango, Nahimana Jonathan.

Simba inayonolewa na kocha Didier Gomes inafikisha alama 64 baada ya ushindi huo katika mchezo wa 26 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu alama tatu zaidi ya mahasimu wao, Yanga SC ambao pia wamecheza mechi tatu zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Post a Comment

0 Comments