Taasisi ya Nyirabu yatoa msaada Tarime

Na Mwandishi Wetu, Tarime

TAASISI ya Nyirabu imetoa msaada wa vitabu vya dini vya Quraan na tende kwa ajili ya waislamu wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Msaada huo, ulitolewa jana na Katibu wa taasisi hiyo, Isaac Nyirabu kwa viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu wilayani (BAKWATA) Tarime.

Akikabidhi msaada huo, Nyirabu alisema wameamua kutoa msaada huo kwa waumini wa dini ya kiislamu kama mchango wao.

"Taasisi inaenzi mambo mazuri yaliyokuwa yakifanywa na mwasisi wake, marehemu Balozi Charles Nyirabu, hivyo msaada huu ni kama kuenzi mchango wake,"alisema.

Alisema, wametoa msaada huo Tarime kama sehemu ya kumuenzi mwasisi wake na kuweka msukumo kwa vijana wa kiislamu kupenda kusoma dini kwa bidii.

''Huu ni utaratibu uliopo kwa kuwa taasisi inafanya shughuli nyingi kwa jamii kama malengo yake, leo tumeanza na waislamu na kesho tunakwenda kwenye dhehebu lingine na makundi pia,''alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Vijana wa BAKWATA wilayani humo, Iddi Maosud, aliipongeza taasisi hiyo kwa msaada huo, ambao wanaamini utakuwa chachu ya vijana kusoma kwa bidii.

"Huu ni msaada mkubwa kwetu, tunaishukuru Taasisi ya Nyirabu, imefanya jambo kubwa na daima huu msaada utakuwa chachu ya kuendelea kumkumbuka mwasisi wa taasisi hiyo,''alisema.

Taasisi ya Nyirabu ni taasisi imeanzishwa kwa ajili ya kusaidia jamii na serikali katika sekta mbalimbali ikiwa ni kuunga mkono juhudi za mwasisi wake, aliyekuwa gavana wa Benki Kuu (BoT) ya Tanzania katika kusaidia jamii.

Post a Comment

0 Comments