🔴𝐋𝐈𝐕𝐄: Uzinduzi wa Kitabu Cha maisha ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi

 

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN NDIYE MGENI RASMI KWENYE UZINDUZI WA KITABU CHA MAISHA YA RAIS MSTAAFU MZEE ALI HASSAN MWINYI KWENYE UKUMBI WA JULIUS NYERERE JIJINI DAR ES SALAAM LEO MEI 8, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 08 Mei, 2021 amezindua kitabu cha maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi kiitwacho “Mzee Rukhsa” ambacho kimeandaliwa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) kupitia mradi wa Tawasifu za Viongozi.

Sherehe za uzinduzi wa kitabu hicho zimefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNICC) na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Philip Mangula, Maspika na Maspika Wastaafu, Majaji Wakuu na Majaji Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Mabalozi, Wabunge, Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu Viongozi Wastaafu, Makatibu Wakuu, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Mhe. Rais Samia amempongeza Mzee Mwinyi kwa kuandika kitabu hicho kwa lugha ya Kiswahili na kubeba maudhui yanayohusu maisha yake binafsi na historia ya Tanzania ambayo inatoa mafunzo mengi kwa Watanzania hasa wenye dhamana za uongozi na kukuza lugha ya Kiswahili Barani Afrika na Dunia nzima.

Kitabu hicho kimezinduliwa katika siku ya kuzaliwa ya Mzee Mwinyi ambapo ametimiza miaka 96, hivyo Mhe. Rais Samia amemtakia heri, afya njema na umri mrefu na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kumtunza wakati wote wa uhai wake.

Amempongeza Mzee Mwinyi kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika kipindi chake cha Urais licha kupokea madaraka hayo makubwa wakati nchi ikiwa katika hali mbaya ya kiuchumi kutokana na madhara ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vita dhidi ya Nduli Idd Amin, ugonjwa wa Ukimwi na masharti magumu yaliyowekwa na taasisi za kifedha za Dunia dhidi ya Tanzania.

Mhe. Rais Samia amesema kupitia kitabu hicho maisha ya Mzee Mwinyi yanatoa mafunzo mbalimbali yakiwemo uongozi ni dhamana, uongozi hautafutwi bali unatoka kwa Mungu, uongozi sio lelemama, uungwana wa kukiri makosa ana umuhimu wa viongozi kupendana na kushirikiana.

Mhe. Rais Samia amempongeza Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Bw. Kadari Singo, na wapigachapa (Mkuki na Nyota) kwa kuandaa kitabu hicho, na pia amemshukuru Balozi wa Finaland hapa nchini Mhe. Dkt. Timo Voipio na wadhamini kwa kufadhili uchapishaji wa kitabu hicho. Ameahidi kufanya uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi hizi karibuni.

Katika salamu zake Mzee Mwinyi amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjaalia afya na neema ya uongozi, amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kukubali kukizindua kitabu hicho na amewashukuru wasaidizi wake wote aliofanyanao kazi akiwemo aliyekuwa mwandishi wake wa hotuba Mhe. Balozi Ombeni Sefue kwa kufanikisha uandishi wa kitabu hicho.

Mchambuzi wa kitabu hicho Prof. Rwekaza Mukandala amepongeza umahiri katika uandishi wa kitabu hicho kilichoeleza maisha ya Mzee Mwinyi aliyezaliwa tarehe O8 Mei, 1925 katika Kijiji cha Kivule, wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani kikiwa na kurasa 491 na utangulizi wake ukiwa umeandikwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamini William Mkapa.

Katika sherehe hizo, Mhe. Rais Samia amemkabidhi Mzee Mwinyi gari ndogo aina ya Mercedes Benz ili kumrahishia kupanda na kushuka baada ya gari alilopewa kuwa refu na hivyo kumpa shida kulitumia. Baada ya sherehe hizo, Mhe. Rais Samia amefuturu pamoja na viongozi waliohudhuria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news