Vigogo wa soka Tanzania watinga robo fainali Azam Sports Federation Cup

Mitanange ya hatua ya 16 bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) imezidi kupamba moto baada ya leo Mei Mosi, 2021 mabingwa watetezi Simba SC kuondoka na alama tatu, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Ni baada ya kuichapa Kagera Sugar 2-1 katika mchezo wa hatua hiyo usiku huu ndani ya dimba la Benjamin Mkapa lililopo Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

Awali Kagera Sugar ilitangulia kwa bao la Erick Mwijage dakika ya 45, kabla ya Simba SC kutoka nyuma kwa mabao ya winga Mghana, Bernard Morrison dakika ya 56 na mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere dakika ya 68.

Simba SC inakuwa timu ya saba kwenda Robo Fainali baada ya Azam FC na Yanga SC za Dar es Salaam kutangulia.

Pia kuna Biashara United ya Mara, Mwadui FC ya Shinyanga, Dodoma Jiji FC ya Dodoma na Rhino Rangers ya Tabora ambayo ni timu pekee isiyo ya Ligi Kuu kufika hatua hiyo.

Awali Dodoma Jiji FC imefanikiwa kutinga Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mabao ya Dodoma Jiji FC yamefungwa na Seif Abdallah Karihe dakika ya 19 na Dickson Ambundo dakika ya 41.

Mapema Yanga SC walifanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mfungaji wa bao hilo pekee ni mshambuliaji Mburkinabe Yacouba Sogne dakika ya 54 akimalizia pasi ya kiungo Mrundi, Said Ntibanzokiza.

Kabla ya Yanga FC, walianza Mwadui FC ambayo ilifanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Mwadui Complex uliopo Kishapu mkoani Shinyanga.

Mabao ya Mwadui FC yalifungwa na Roshwa Rashid dakika ya 14 na Wallace Kiango dakika ya 24.

Wakati huo huo Azam FC ilitangulia kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo dakika za 25 na 65, wakati la Polisi limefungwa na Marcel Boniventura Kaheza dakika ya 76 kwa penalti.

Mbali na hayo hatua ya 16 Bora ya ASFC itakamilishwa Mei 2, 2021 kwa mchezo kati ya JKT Tanzania na Namungo FC Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments