Basi la Kampuni ya Classic laua, wajeruhiwa kutoka Kampala kwenda Dar

Watu wanne wamekufa na wengine watano wakipata vilema vya maisha kutokana na ajali ya basi la Kampuni ya Classic lenye namba za usajili SRC 3 lililokuwa likitokea Kampala nchini Uganda kuelea jijini Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka huko katika kijiji cha Buyubi wilaya na Mkoa wa Shinyanga.
Ajali hiyo imetokea usiku wa leo Saa 10 alfajiri ambapo basi hilo lilikuwa likitokea Jijini Kampala nchini Uganda kuelekea Jijini Dar es salaam, ambapo baadhi ya abiria wameeleza kuwa dereva wa basi hilo alikimbia baada ya ajali.

Baadhi ya majeruhi wamesema kuwa ajali hiyo imetokea baada ya dereva kushindwa kukata kona katika barabara ya Kahama-Shinyanga katika njia panda ya Didia.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa baadhi ya abiria waliokuwemo kwenye basi hilo ni wanafunzi wanasoma nchini Uganda ambao walikuwa wakisafiri kuja likizo Tanzania.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na hospitali ya misheni Bugisi kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amewataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Wahda Yussuf mkazi wa Pemba, Josephine Joseph mkazi wa Dar es Salaam, Rehema Hajji mkazi wa Jang’ombe Zanzibar na Nassor Juma mkazi wa Zanzibar.

Kamanda Magiligimba pia amewataja waliopata vilema vya maisha baada kukatika viungo vyao vya mwili kuwa ni Njama Hassan ambaye amekatika mkono wake wa kushoto, Mohamed Daudi, amekatika mkono wa kulia, Fatuma Kessy amekatika mkono wa kushoto, Saada Mmanga amekatika mguu na mkono wake wa kushoto.

Akifafanua Kamanda huyo wa Polisi alisema ajali hiyo ilitokea saa 10.50 usiku wa kuamkia jana huko katika kijiji cha Buyubi, Kata ya Puni wilayani Shinyanga baada ya basi hilo lililokuwa likiendeshwa na dereva Mackson Mkulu kuacha njia na kupinduka.

Amesema, mbali ya watu waliopoteza maisha na waliokatika viungo vya miili yao pia abiria wengine 27 walijeruhiwa kati yao 15 walitibiwa katika kituo cha Afya Didia na kuruhusiwa na wengine 12 walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili kuchunguzwa afya zao.

“Chanzo cha ajali hii ni mwendo kasi aliokuwa nao dereva na hivyo kushindwa kulimudu gari alilokuwa akiendesha lilipofika kwenye kona kutokana na hali hiyo liliacha njia na kupinduka, na baada ya ajali hiyo dereva ametoweka na kutokomea kusikojulikana, tunamsaka ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la kuendesha gari kwa mwendo kasi.

“Nirejee kutoa wito kwa madereva wote hasa wale wanaoendesha mabasi yanayosafirisha abiria kuendesha magari yao kwa mwendo unaoruhusiwa kwa mujibu wa sheria, hatutosita kumchukulia hatua za kisheria dereva ye yote atakayebainika kutoheshimu sheria za barabarani zilizopo,” ameeleza Kamanda Magiligimba.

Mmoja wa abiria walionusurika katika ajali hiyo, Fortunace Wilbard mkazi wa Dar es Salaam alisema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva kushindwa kuimudu kona kali katika eneo hilo la kijiji cha Buyubi na kwamba kabla halijapinduka liliyumba na kisha kuanguka.

“Nahisi ilikuwa inakaribia saa 11 alfajiri hivi, nilikuwa macho, ghafla niliona gari limeyumba kidogo kama vile dereva alikuwa anakwepa kitu, lakini baada nikaona linaendelea kulalia upande mmoja na muda mfupi likapinduka, watu watatu walifia palepale ndani ya gari na mmoja njia wakati akikimbizwa hospitali,”amesema Wilbard.

Wilbard amesema, sehemu kubwa ya abiria waliokuwemo ndani ya basi hilo ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bugema kilichopo Kampala nchini Uganda ambao walikuwa wakirejea nyumbani kwa ajili ya likizo

Post a Comment

0 Comments