Jalada la kutekwa Bilionea Mohammed Dewji lafikishwa kwa DPP mpya

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jalada la kesi la tuhuma za kumteka mfanyabiashara wa Kitanzania, Bilionea Mohammed Dewji (MO) inayomkabili dereva teksi, Mousa Twaleb limefikishwa mbele ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya maelekezo baada ya kuchukua muda mrefu sasa.

Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah alidai hayo Juni 3, 2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mmahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo Jijini Ilala mkoani Dar es Salaam, Huruma Shaidi.

Ni baada ya kudai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na pia jalada la kesi hiyo lilifikishwa mbele ya DPP mpya, kwa sababu ni moja ya kesi ambazo zimechukua muda mrefu bila kuendelea.

Aidha, baada ya Ngukah kudai hayo, Wakili wa mshtakiwa huyo, Mahfudhu Mbagwa alidai kuwa Machi 24,2021 upande wa mashtaka ulidai wamemkamata mshtakiwa mwingine Afrika ya Kusini, wanafanya utaribu wa kumleta nchini Tanzania.

Wakili Mbwaga aliendelea kudai kuwa, kwa hatua iliyofikia sasa, hatua zingine zinatakiwa kuendelea kwa mshtakiwa ambae yuko mahakamani, kwa sababu hakuna kinachoendelea kwa sasa.

Akijibu hoja hizo, Ngukah alidai, shauri hilo ni la uhujumu uchumi na Wakili Mbagwa anataka Mahakama itoe amri kwenye kesi hiyo wakati kwenye kesi ya uhujumu uchumi ni hadi DPP atoe kibali cha kusikilizwa na ni baada ya upelelezi kukamilika.

Ngukah amesema kuwa,hii kesi ni moja ya kesi ya muda mrefu, "ambazo tumezifikisha mbele ya DPP kwa sababu yeye ndiyo mwenye kushtaki na kufuta,"alidai.

Akijibu hoja ya mshtakiwa aliyekamatwa Afrika Kusini, Ngukah alidai kuwa ni kweli alichokidai wakili kuwa kuna mshtakiwa alikamatwa na wapo kwenye utaratibu wa kumleta Tanzania.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Shaidi amesema ni kweli kesi hiyo ni ya muda mrefu na haiendelei mbele, ambapo katika kikao ambacho wamekifanya hivi karibuni kilichoudhuriwa na wawakilishi wa DPP aliipendekeza hiyo kesi kwa ajili ya hatua zaidi.

"Kwenye kesi yako niliitolea mfano ni kesi ambayo sijaridhika nayo, kama wewe unakosa lako basi liendelee na wale washtakiwa wengine wakikamtwa basi na wao washtakiwa sio wewe una kaa tu gerezani ukisubiri wao wakamatwe,"amesema Hakimu Shahidi

Hakimu huyo, alikwenda mbali zaidi kuwa kama imeshindikana kwa mshtakiwa kushtakiwa kwa kosa lake, basi aachiwe kwa kupewa dhamana ya polisi wakati anasubiri wengine wakamatwe. Aidha, kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 16,2021 kwa ajili ya kutajwa tena.

Hhata hivyo, baada ya hakimu kusema hayo, mtuhumiwa Twaleb alinyoosha mkono na kumueleza hakimu kuwa, hakumteka Mohamed Dewji na wala Dewji mwenyewe hamfahamu, kwa hiyo hajui kinachoendelea kwake.

Watuhumiwa wengine ambao upande wa mashitaka inawatafuta ni raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini wanaodaiwa kumteka mfanyabiashara huyo.

Washitakiwa hao ambao ni Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.

Katika kesi hiyo inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, 2018, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia, inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo ya Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara Mohamed Dewji kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.


Aidha, inadaiwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Mfanyabiashara Bilionea, Mohamed Dewji alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments