Rais Macron amtunuku Balozi Radhia Msuya Nishani ya heshima

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amemtunukia Balozi Radhia N. Msuya wa Tanzania, nishani ijulikanayo kama “National Order of Merit”.
Balozi Msuya amevikwa nishani hiyo na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mheshimiwa Frederick Clavier.

Hafla fupi ya kumtunuku Balozi Msuya nishani hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Balozi Radhia N. Msuya ametunukiwa nishani hiyo kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Ufaransa wakati akiwa Mkurugenzi wa Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2006-2010).

Ametambuliwa kwa mchango mahsusi aliyoutoa wakati Ufaransa ilipokuwa Rais wa Umoja wa Ulaya.
Nishani hiyo ilianzishwa mwaka 1963 kwa nia ya kutambua mchango wa watunukiwa wake katika kuendeleza ushirikiano na Ufaransa hasa katika ustawi wa dunia. Baadhi ya watu mashuhuri waliowahi kutunukiwa nishani hiyo ni Rais François Mitterrand wa Ufaransa; Mfalme Juan Carlos I wa Uhispania na Bw. Njoroge Mungai wa Kenya.

Balozi Radhia ni mwanadiplomasia aliyefanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 35. Ambapo alishika nafasi mbali katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, uliopo New York, Marekani na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Mwaka 2010 mpaka 2016 Balozi Radhia aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, akisimamia masuala ya SADC, Botswana, Lesotho na Namibia.

Mwaka 2017 Balozi Radhia Msuya alipata uhamisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kama Msaidizi wa Katibu Tawala. Nafasi hii aliitumikia hadi alipostaafu utumishi wa umma mwaka 2018.

Kwa sasa Balozi Radhia Msuya yuko katika kampuni binafsi ya ushauri inayojishughulisha na masuala ya uwekezaji na diplomasia ya uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news