Ujumbe rasmi kutoka kwa Gerson Msigwa kwenda kwa Jaffar Haniu na wadau

Anaandika aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali...Nakutakia kila la kheri Ndg. yangu Jaffar Haniu. Mwenyezi Mungu akuongoze na kukusimamia katika jukumu hili.
Awali ya yote naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na baraka tele alizonijaalia wakati wote. Ameniongoza na kunilinda kila hatua bila kikomo, na bado yupo nami. Sifa na utukufu ni kwake.

Namshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini kwanza kuniteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali na pili kunikaimisha Ukurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu kwa takribani miezi miwili. Naahidi sitamuangusha.

Pia, namshukuru Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu kwa kipindi chake chote cha Urais. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpumzisha mahali pema peponi, mpaka tutakapoonana tena Inshaallah.

Halikadhalika naomba kumshukuru Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ambaye aliniamini kwa uteuzi wa kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi ulionitoa Songea Mkoani Ruvuma nikiwa Mwandishi wa Habari wa TBC na kuja Ikulu Dar es Salaam. Mwenyezi Mungu aendelee kukupa afya njema na umri mrefu ili tuendelee kufaidi busara zako.

Napenda kuwashukuru nyote kwa ushirikiano na upendo mkubwa tuliokuwa nao katika kipindi chote cha Miaka 5 na Miezi 6 ambacho nimekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Haikuwa rahisi lakini kwa ushirikiano wenu na kwa mapenzi ya Mungu tumefanya yote ambayo tumeyafanya.

Kwa namna ya pekee nawashukuru waandishi wa habari wenzangu, wamiliki wa vyombo vya habari na wote ambao majukumu yangu yaliwategemea zaidi.

Naomba niwakaribishe Idara ya Habari (MAELEZO). Nipo vizuri na timamu kwa kazi.

Mwisho nasema “Shughuli ni watu na watu wenyewe ndio sisi” Tuchape kazi kwa juhudi na maarifa kama ambavyo @samia_suluhu_hassan anatutaka. 

Post a Comment

0 Comments