Waziri Ndumbaro: Matukio ya ujangili yamepungua nchini

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amesema kuwa, matukio ya ujangili nchini yamepungua kwa asilimia 90 kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali, ANARIPOTI DOREEN ALOYCE.

Dkt.Ndumbaro amesema hayo Bungeni jijini hapa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Amesema, katika kukuza uchumi,wizara yake imeendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali za maliasili kwa kudhibiti ujangili, biashara haramu ya nyara, uvunaji haramu wa mazao ya misitu na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.

"Matokeo ya sensa ya mwaka 2020 yameonesha kuongezeka kwa idadi ya tembo katika mfumo ikolojia Serengeti kutoka 6,087 mwaka 2014 hadi 7,061 mwaka 2020,"amesema.

Amesema, licha ya hayo kuna mafanikio ya kupungua kwa ujangili, uvunaji haramu wa mazao ya misitu na kuongezeka kwa wanyamapori ambayo yamechangiwa pamoja na mambo mengine, kuendeshwa kwa siku doria 746,413 zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 5,609.

"Hata hivyo mitandao 95 ya ujangili imevunjwa na kuzuiliwa kwa matukio 302 ya ujangili kabla hayajatendeka,"amesema.

Ametaja jitihada nyingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa minara mitatu ya mawasiliano ya redio katika maeneo 15 ya Oldeani, Losirwa na Kreta ya Empakai.

Kutokana na hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi,Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Kwezi ametoa maoni na ushauri wa kamati akisema kwa kuzingatia uchambuzi uliofanywa na kamati hiyo wanatoa mapendekezo katika maeneo ya Mwenendo wa upatikanaji wa fedha, Makusanyo ya Maduhuli,Bajeti ya Maendeleo na Uendeshaji wa Shughuli za utalii. 

Ameeleza kuwa, kumekuwepo kwa mwenendo usioridhisha wa upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo katika bajeti inayoidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, jambo ambalo limepelekea wizara kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kusimamia sekta nzima ya Maliasili na Utalii.

Hivyo Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha kuwa, fedha zinazotengwa katika bajeti ziwe zinatolewa kwa kiasi kinachotosheleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Licha ya hayo, Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa, kwa kufanya hivi, wizara itakuwa na uwezo wa kupanga kulingana na vipaumbele vya utekelezaji wa majukumu yake.

"Makusanyo ya maduhuli katika Sekta ya Utalii kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kumekuwa na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa maduhuli katika wizara na taasisi zake, kutokana na changamoto hiyo kumepelekea kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na namna ya taasisi hizo kujiendesha zenyewe,"amesema.

Kwezi amesema,kamati hiyo inashauri wizara kupitia taasisi na idara zake ziwawekee malengo wakuu wa taasisi na idara zote zilizochini yake na malengo ya makusanyo kwa kila robo mwaka na malengo hayo yawe ndio kipimo cha utendaji kazi wao. Pia amesema, wizara ibuni mikakati endelevu ya ukusanyaji wa mapato.

Hatua hiyo ni pamoja na kushirikiana na Wizara ya Elimu, Tamisemi na Ofisi ya Waziri Mkuu, katika kuratibu namna bora kupata watalii wengi wa ndani hususani wabunge, taasisi na idara mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali, mikoa na halmashauri za wilaya zote, vyuo, wanafunzi wa sekondari na shule za msingi.

Aidha, wizara kuainisha changamoto zilizopo katika utaratibu uliopo wa ukusanyaji wa mapato ya wizara na kuziwasilisha katika kamati kwa ajili ya kutolea mapendekezo.

Post a Comment

0 Comments