DC wa Handeni atoa wito kwa wadau kushirikiana kuinua viwango vya elimu Tanga

Na Yusuph Mussa, Handeni

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Siriel Nchemba amesema ili kukuza kiwango cha elimu Mkoa wa Tanga ni lazima wadau wote ikiwemo sekta binafsi kushiriki kwenye mchakato huo, kwani suala la elimu ni mtambuka, na linahitaji uwajibikaji wa pamoja kulifanikisha.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati anaweka jiwe la msingi Kituo cha kulelea watoto wadogo cha Lungo Day Care kilichopo Mtaa wa Komsanga, Kata ya Vibaoni katika Halmashauri ya Mji Handeni.

Nchemba amesema, kituo hicho ambacho pia kitatoa elimu ya awali na msingi kwa mchepuo wa kiingereza, kitakuwa na uwezo mkubwa wa kuwajenga mapema watoto wadogo kielimu, na wataweza kuingia darasa la kwanza na kuweza kujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

"Ili kukuza elimu katika mkoa wetu wa Tanga na hasa wilayani kwetu Handeni, kunahitajika ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi. Hiyo itasaidia kukuza elimu na kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maendeleo.

"Kituo hiki ambacho pia kitatoa elimu kwa mchepuo wa kingereza, kitakuwa na uwezo mkubwa wa kuwajenga mapema watoto wadogo kielimu, na wataweza kuingia darasa la kwanza na kuweza kujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Hivyo ni matumaini yangu wananchi watachangia kituo hiki ili kiweze kukamilika, na mimi nachangia kabisa matofali 100 kwa kutoa sh. 120,000,"amesema Nchemba.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Hashimu Lungo amesema lengo kubwa la kuanzishwa kituo hicho ni kuhakikisha wanasaidia malezi ya watoto wadogo wa umri kati ya miaka miwili hadi mitano, wakiwa wamelenga kumpatia mtoto makuzi mazuri na elimu.

"Kituo kimelenga kutoa malezi ya mchana kwa watoto ili kusaidia ukuaji wa mtoto na kuhakikisha watoto wanahudumiwa bila kufanyiwa ukatili wa namna yeyote ile. Kwa hiyo kituo kikikamilka kitahakikisha kinatoa ulinzi kwa watoto wote kwa wakati wote ambao watoto watakuwa hapa.

"Kituo kitasaidia kutoa ajira kwa walezi na waangalizi wa watoto. Tutaajiri wapishi, tunatarajia kuajiri walimu walezi na watumishi wengine kadiri ya mahitaji ya kituo yatakavyo kuwa. Na tunatarajia kuwa walipa kodi wazuri na kuchangia pato la Taifa, na kituo kikienda vizuri, kitamsaidia mama kupunguza majukumu ya ulezi,"amesemaema Lungo.Soma hapa: Picha zinazohusiana.

Lungo ambaye ni fundi seremala wilayani Korogwe, alisema pia wanatarajia kuanzisha shule ya awali na msingi ili kuchangia maendeleo ya jamii zote katika elimu na makuzi, na hadi sasa Lungo Day Care imefanikiwa kujenga miundombinu michache kwa kuanzia wamejenga darasa moja, ofisi moja, chumba cha kulala ama kupumzika watoto na chumba cha kuishi mwalimu au mhudumu wa watoto.

"Pamoja na jitihada hizo, tunakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile matofali 300 (block) na mifuko ya saruji nane kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa darasa ili tuweze kuanza na darasa tukisubiria miundombinu mingine kukamilika ambayo ni madarasa mawili, ukumbi na nyumba ya mapumziko.

"Lakini pia tuna changamoto ya kutofika kwa umeme, maji pamoja na barabara. Tunakuomba Mkuu wa Wilaya, tusaidie watoa huduma husika wafike na kutupatia huduma hiyo kama wateja wengine, na tupo tayari kuchangia kadri watakavyoona. Hii itaboresha utoaji huduma kwa watoto," alisema Lungo.

Post a Comment

0 Comments