Fainali ya kibabe Copa America kati ya Brazil na Argentina

NA GODFREY NNKO

Mlinda mlango wa Aston Villa, Emiliano Martinez ameiwezesha timu yake ya Taifa ya Argentina kutinga fainali katika michuano ya Copa America.
Picha na Getty images.

Ni baada ya mtanange uliopigwa usiku wa kuhamkia leo ambapo Argentina walikutana na Colombia huku dakika tisini zikimalizika kwa suluhu ya moja moja.

Uzio wa Martinez uliwezesha timu yake kuibuka kwa mabao 3-2 kupitia mikwaju ya penaliti. Ambapo aliokoa mikwaju mitatu kati ya mitano, hivyo kuwapeleka hadi fainali.

Timu yake ilifanya kweli kupitia kazi nzuri za Lionel Messi, Leandro Paredes na Lautaro Martinez, hivyo kuifanya ndoto ya Argentina kwenda kutafuta kikombe dhidhi ya Brazil kutimia.

Mtanange ulianza kwa Argentina kufungua kwa bao la kwanza ndani ya dakika saba kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Gio Lo Celso kwa ushirikiano wa Messi na Lautaro Martinez.

Argentina walionekana kuutawala mpira huo, huku matarajio yakiwa wangeweza kupachika bao la pili kipindi cha kwanza. Lakini mambo hayakwenda hivyo.

Ndipo kocha wa Colombia, Reinaldo Rueda akafanya mabadiliko mara tatu, hali iliyoongeza ufanisi na uwezo.

Colombia ilionekana kuwa kizuizi kwa mipango ya Argentina, kwani ndani ya dakika 61 walifanya jambo lao. Ingawa matarajio hayakufikiwa.

Kwa sasa Argentina na Brazil zitakutana Jumamosi usiku huko Mracana mjini Rio de Janeiro kujua nani atabeba ndoo.

Awali, Lukas Paquetta ndani ya dakika 35 amezitumia kuwapa heshima mabingwa watetezi wa Copa America ambayo ni timu ya taifa ya Brazil.

Ni bao pekee ambalo limewaangusha Peru katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Julai 6,2021.

Kwa sasa Brazil ndiyo ambao wanapewa kipaumbele cha kubeba taji hilo.

Paquetta anakuwa mwamba kwa Brazil chini ya kocha Tite kwani katika mechi ya robo fainali dhidi ya Chile goli pekee alilolifunga lilitoa nafasi kwa Selcao kutinga nusu kabla tena ya goli lake kufika fainali.

Post a Comment

0 Comments