Yanga SC:Tunakwenda kuwamaliza tena Simba SC pale Lake Tanganyika

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Fredrick Mwakalebela amesema baada ya ushindi dhidi ya Simba SC kwenye mchezo uliopigwa Julai 3, mwaka huu kwenye Dimba la Mkapa lililopo Halmashuri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam wapo tayari kwa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba, Julai 25, mwaka huu.

Awali Yanga SC iliifunga Simba SC bao 1-0 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo timu hizo zitakutana katika fainali ya Kombe la Shirikisho Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Kipigo cha hicho kinakumbushia machungu ya kichapo cha Machi 8, mwaka jana 1-0 pia hapo hapo Benjamin Mkapa bao pekee la Mghana ambaye sasa amehamia Simba, Bernard Morrison dakika ya 44, mchezo ambao ulihudhuriwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Aidha, kwa mwaka huu, Yanga SC imeipa kipigo cha pili Simba pamoja na ushindi wa Januari 13 wa penalti 4-3 kufuatia sare ya 0-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.
“Mechi ya ligi ilikuwa ni ya kutafuta heshima na tumefanikiwa kuwafunga Simba, hivyo mechi ya Kigoma tunakwenda kufanya kazi na nina imani tutalitwaa Kombe la Shirikisho,“amesema Mwakalebela.

Ameongeza kuwa, "Tunajua udhaifu wa Simba ulipo ndiyo maana wamekuwa wakisumbuka kupata matokeo mbele yetu kwa msimu wa pili mfululizo.

"Benchi la ufundi, wachezaji pamoja na viongozi tunafanya kazi kwa kushirikiana ndiyo maana tumeweza kulifanikisha hili na Kigoma pia tutakwenda kufanikiwa, kikubwa mashabiki wazidi kutuunga mkono,"amesema.

Post a Comment

0 Comments