Moto wateketeza bweni la wasichana wa Shule ya Sekondari Kiwangwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Janga la moto limezidi kuzikumba shule na taasisi mbalimbali nchini, ambapo moto
umezuka ghafla kwenye bweni la wasichana wa Shule ya Sekondari Kiwangwa na kuteketeza vifaa mbalimbali vya wanafunzi.
Moto huo unadaiwa kutokea majira ya saa usiku wa kuamkia leo Julai 23, 2021.

Mbunge wa Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete kuwa, kwenye bweni hilo walikuwa wanalala wanafunzi wa kike 90 na kwamba wote ni wa kidato cha nne.

Mheshimiwa Ridhiwani amesema, wakati moto huo ukitokea, wanafunzi hao walikuwa kwenye masomo ya ziada ya usiku.
"Ni kweli tumepata maafa haya bweni limeungua na limeungua kweli kweli kama unavyoona kwenye picha cha kumshukuru Mungu nimeambiwa wanangu wapo salama, nakimbizana sasa tujue namna ya kuwasaidia haraka maana wapo kwenye maandalizi ya mitihani ya kidato cha nne, hatutaki tuwaangushe kwa sababu ya adha hii," amesema Ridhiwani.

Hivi karibuni Serikali ililazimika kuifunga kwa muda wa siku 14 Shule ya Sekondari Geita kutokana na matukio ya kuungua moto mara tatu mfululizo.

Uamuzi huo ulitolewa Julai 14,2021 baada ya kuungua moto siku moja kabla ikiwa ni mara ya tatu ndani ya siku saba. 

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemery Senyamule alitangaza uamuzi huo baada ya moto kuteketeza bweni na kujeruhi wanafunzi watatu.

Katika tukio la kwanza lililotokea Julai 5,2021, moto uliteketeza magodoro na masanduku ya wanafunzi, la pili likatokea Julai 6 kwa kuteketeza maabara mbili za sayansi.

Post a Comment

0 Comments