NCCR Mageuzi, ACT Wazalendo, CUF watoa tamko kukamatwa viongozi wa CHADEMA



Wakati huo huo Chama Cha Wananchi (CUF) kimelaani maamuzi ya Jeshi la Polisi nchini kuingilia kwa lengo la kuzorotesha harakati halali zenye dhamira ya kuimarisha Demokrasia na Utawala wa Sheria nchini.

Hivi karibuni jeshi la Polisi limezuia mikutano ya hadhara ya CUF- Chama Cha Wananchi iliyopangwa kufanyika Manzese, Vingunguti na Temeke kwa maelezo kwamba mikutano ya hadhara bado haijaruhusiwa na Rais na pia mikusanyiko hairuhusiwi kutokana na janga la CORONA. 

Aidha jeshi la Polisi limezuia Kongamano la CHADEMA la kudai Katiba mpya lililokuwa lifanyike Mwanza Julai 21 mwaka huu, pamoja na kuwakamata viongozi waandamizi wa akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe.

CUF- Chama Cha Wananchi kinapinga vitendo hivi vya Jeshi la Polisi ambavyo bila shaka vinatokana na maelekezo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kufuatia matamko yake aliyoyatoa wakati wa kuadhimisha siku 100 za kuwa madarakani.

Tunatahadharisha kwamba vitendo hivi visipodhibitiwa mapema vinaweza kuliingiza taifa kwenye vurugu na uvunjifu wa amani, na Rais Samia hatokwepa lawama kwa kuwa mikutano ya hadhara na makongamano ambayo Serikali anayoiongoza inavizuia vimeruhusiwa na Katiba na Sheria zingine za nchi alizoapa kuzilinda.

Tunaikumbusha Serikali na kutoa wito kama ifuatavyo:-

(i) Virusi vya CORONA havibagui kwa hiyo hata ile mikutano inayomhusisha Rais au viongozi wengine wa Serikali au wa CCM ni mikutano hatarishi. Hivyo kuzuia mikusanyiko inayohusu vyama vya upinzani na kuruhusu ile ya CCM na Serikali ni kukandamiza Demokrasia na ni kinyume na Utawala Bora unaozingatia Sheria.

(ii) Jeshi la Polisi lingeweza kumkamata Mhe. Mbowe popote hata alipokuwa msibani, kama kweli kuna tuhuma zozote dhidi yake. 

Kumkamata kufuatia Kongamano lao la Mwanza na kisha kudai kwamba anatuhumiwa kwa ugaidi ni jambo linaloibua maswali mengi bila majibu. 

Tunakumbuka jinsi Rais Samia alivyotoa msisitizo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuziondoa kesi zote za kubambikiza katika kipindi ambacho yeye alikuwa Ikulu kama Makamu wa Rais. 

Pamoja na kupata faraja kupitia msimamo wake huo, lakini hiyo kauli ni taarifa kwa watanzania kwamba kuna ubambikaji mkubwa wa kesi hapa nchini. 

Tunatoa tahadhari kwa Serikali kutovitumia vyombo vyake kubambikiza kesi kwa Lengo la kutaka kuzuia Sauti ya Umma katika kupambania masuala ya msingi. Ni vema na haki Serikali ikahakikisha haki inatendeka na Utawala wa Sheria unaenziwa.

(iii) Rais anapaswa kutamka kwamba mikutano ya hadhara na makongamano ni halali Kisheria na kwamba Vyama vya Siasa viko huru kuendesha mikutano na makongamano bila kubughudhiwa. 

Tunamkumbusha Rais kwamba tuliingia kwenye Uchaguzi Mkuu uliovurugwa na Serikali ya CCM 2020 tukiwa katikati ya wimbi la maambukizi ya CORONA. Watanzania wakumbushwe tu njia za Kitaalam za kujikinga na maambukizi wakati harakati zingine zikiendelea kwa kuchukua tahadhari.

CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa Serikali kupitia jeshi la Polisi kuwaachia viongozi wote wa CHADEMA wanaoshikiliwa kufuatia Kongamano la Mwanza.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Prof. Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti Taifa
CUF- Chama Cha Wananchi
Julai 23, 2021

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news