Mzee wa Upako afunguka kuhusiana na utoaji chanjo ya Corona

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo (Mzee wa Upako) ametoa wito kwa Watanzania kuwa na imani na Serikali kuhusiana na utoaji chanjo ya ugonjwa wa corona.

Mzee wa Upako ametoa rai hiyo leo Jumatano Julai, 28, 2021 katika hafla ya uzinduzi wa chanjo ya covid–19 iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema ili kupambana na janga hilo lililokumba ulimwengu mzima ni lazima nchi iwe na umoja na kushirikiana kwa pamoja kwani Serikali imejiridhisha vya kutosha juu ya chanjo hiyo.

“Wote tunakubali kwamba corona ni vita na hatuwezi kuishinda kama hatuna umoja, tuna Wizara ya Afya, Waziri Mkuu yupo sidhani kama hawa wenzetu wanaweza kuitoa nchi kafara kwamba watu wapate chanjo halafu wafe, lazima mifumo ya nchi yetu imejiridhisha, haitakuwa 100 kwa 100 kila kitu kina mapungufu lakini tujenge imani.

“Mimi ni muhubiri wa zamani nilianza kuhubiri injili wakati wa Kambarage niwaombe maaskofu wenzangu tujenge imani kwa Serikali yetu na Wizara ya Afya, tunachanja kwa nia njema kwa ajili ya afya zetu, watakaosema Mzee wa Upako anajipendekeza sawa tu kwani akutukanaye hakuchagulii tusi,” amesema.

Ameongeza kuwa, watu walimnukuu vibaya Hayati Dkt. John Magufuli kwani hakusema watu wasichukue chanjo bali umakini uwepo na kwamba tayari wameshajiridhisha kuwa nchi itakuwa salama

“Uzuri Tanzania ni nchi ya ajabu katika Bara la Afrika hivyo tusiogope wala kufadhaika kwani tunafanya haya kwa nia njema,” amesema Mzee wa Upako.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news