NMB YAZIKOMBOA SHULE KISARAWE, YAMWAGA MSAADA WA MILIONI 10/-

Na Rotary Haule,Kisarawe

BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati 165 pamoja na viti na meza 50 wenye thamani ya Sh.milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule mbili zilizopo wilayani Kisarawe Mkoa Pwani.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Serikali kutoka Benki ya NMB, Vicky Bishubo akimkabidhi msaada wa meza na viti kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais ,Muungano na Mazingira, Selemani Jafo kwa ajili ya kusaidia shule mbili zilizopo wilayani Kisarawe,msaada huo umetolewa juzi wilayani Kisarawe ukiwa na thamani ya sh.milioni 10,anayeshuhudia katika ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzenga, Upendo Fihi.(Picha na Rotary Haule).

Msaada huo umekabidhiwa juzi kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Chanzige A' iliyopo Kisarawe Mjini.

Awali akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Serikali kutoka NMB Vicky Bishubo,alisema kuwa kutolewa kwa msaada huo kulitokana na maombi yaliyopokelewa kutoka wilayani humo.

Bishubo alisema kuwa, baada ya kupokea maombi hayo hawakusita kuyafanyia kazi na kwamba benki iliridhia kutoa mabati msaada huo ikiwa ni mpango wake wa kurudisha sehemu ya faida kwa jamii na wanafanya hivyo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu na afya.

Aidha ,Bishubo alisema pamoja na msaada huo lakini NMB imeendelea kutenga fedha kwa asilimia moja kwa ajili ya kuunga mkono Serikali katika kusaidia kwenye sekta ya elimu na afya na kwamba mpaka sasa tayari imetoa msaada wa zaidi ya Sh. bilioni 1 nchini.

Bishubo,aliongeza kuwa kwa mwaka 2021/2022 benki tayari imetenga kiasi cha Sh .bilioni 2 ambazo zitakwenda kwa jamii kupitia misaada mbalimbali katika sekta ya elimu na fedha .

"NMB inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha miundombinu ya elimu na afya na leo hii tupo hapa kwa ajili ya kutoa msaada wa bati 165 na viti 50 zenye meza zake kwahiyo tunaomba mpokee," alisema Bishubo.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Serikali kutoka Benki ya NMB, Vicky Bishubo wa nne kutoka kushoto akimkabidhi mabati 165 Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais ,Muungano na Mazingira Selemani Jafo(kulia) hafla iliyofanyika juzi katika viwanja vya Shule ya Msingi Chanzige A ' iliyopo Mjini Kisarawe ,msaada huo utatumika kwa ajili ya kupaua Shule hiyo.(Picha na Rotary Haule).

Bishubo,aliipongeza Serikali kwa namna ambavyo inaungana mkono na kutoa ushirikiano kwa NMB na ameomba ushirikiano huo uendelee ili kuweza kufikia malengo ya benki na hata malengo ya Serikali katika kuwahudumja jamii.

Alisema mpaka sasa NMB inajumla ya matawi 226 ,huduma za ATM 800 ,Mawakala 9000 na kusema lengo lake ni kuwafikia Watanzania wengi wakiwemo wa juu na wachini wakiwemo wakulima.

Kwa upande wake Waziri Jafo aliishukuru benki ya NMB kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusaidia jamii hususani katika masuala ya elimu na afya.

Jafo,alisema NMB imekuwa benki ya mfano na Watanzania wanajivunia benki hiyo huku akisema kwa upande wa Kisarawe imekuwa na msaada mkubwa kwakuwa wamekuwa wakisaidia mara kwa mara.

Alisema kuwa,katika msaada huo bati 165 zitasaidia kupaua Shule ya Msingi Chanzige A ,na viti 50 vitakwenda katika Shule ya Sekondari Mzenga jambo ambalo limeleta faraja kwake.

"Hakika nimefurahishwa na benki hii ya NMB kwa kutoa msaada huu maana kila ninapoomba napewa na leo napewa bati na meza kwahiyo sina budi kusema watu wajiunge na NMB kwakuwa ndio benki ya jamii,"alisema Jafo.

Hata hivyo,mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mzenga Upendo Fihi aliishukuru NMB na kusema msaada huo utawasaidia kusoma katika mazingira mazuri lakini wasichoke kwakuwa shule yao bado inakabiliwa na changamoto ya maji na vitabu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news