Profesa Lipumba awa wa kwanza kupata chanjo ya Corona Dar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Leo Julai 22, 2021 Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa Profesa Ibrahim Lipumba, amekuwa kiongozi wa kwanza wa kisiasa nchini kujitokeza hadharani na kupata chanjo ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19).

Mheshimiwa Profesa Lipumba amepata chanjo hiyo katika Kliniki ya Umoja wa Mataifa iliyopo Masaki mkoani Dar es Salaam.

Haya yanajiri ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata chanjo hiyo hapa nchini.

Majaliwa aliyabainisha hayo katika Msikiti wa Mtoro uliopo jijini Ilala, Dar es Salaam katika katika Baraza la Eid El Adha.

“Chanjo hiyo ipo tayari nchini, mwananchi yoyote anayetaka kuchanjwa akachanje kwa ajili ya kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo,”alibainisha Waziri Mkuu.

Akizungumza na waandishi baada ya kutoka kupata chanjo hiyo, amesema amejikuta akipata nafasi hiyo kupitia mke wake, Gojina Mtenga, anayefanya kazi Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Watoto Duniani (Unicef), Cox Bazaar nchini Bangladesh.

"Kama mlivyosikia wenzetu wa mashirika haya ya kimataifa wameruhusiwa kuanza kupata chanjo hizi pamoja na familia zao.

"Hivyo na mimi kupitia mke wangu ndio imeniwezesha leo kuja kupata chanjo hii hapa na nilipata taarifa usiku wa jana ikinitaka nifike hapa leo saa tano asubuhi nashukuru kwa kulikamisha hili, "amesema Profesa Lipumba.

Hata hivyo amesema baada ya chanjo hiyo ya awali anatakiwa arudi tena baada ya wiki sita mpaka nane kupata chanjo ya pili ili kukamilisha chanjo nzima ya kujikinga ya kujikinga na ugonjwa huo.

Pia mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuchangamkia chanjo hiyo ili kuwa salama.

Wakati kwa upande wa Serikali ameishauri iangalie namna ambayo itawezesha wananchi wanaougua ugonjwa huo kupata matibabu yake kwa gharama nafuu.

Post a Comment

0 Comments