Taasisi ya Kulinda Amani Tanzania yawapa tabasamu wagonjwa

Na Rachel Balama, Diramakini Blog

Taasisi ya Kulinda Amani Tanzania (TPF) imetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh.milioni 1.5 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa katika Hospitali nne zilizopo jijini Dar es salaam.
Mbali na misaada hiyo pia wanachama wa taasisi hiyo wamechangia damu ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu katika hospitali hizo.

Hospitali zilizopata msaada ni pamoja na Mwananyamala vifaa vyenye thamani ya sh. 620,000, Amana vifaa vya sh. 280,000, Temeke vifaa vyenye thamani ya sh. 120,000 na Vijibweni iliyopo Kigamboni vifaa vyenye thamani ya sh. 400,000.

Baadhi ya vitu iliyotolewa ni pamoja na sabuni za maji,sabuni za unga, miswaki, kanda mbili, pampasi, dawa za meno, mashine ya kupimia presha, kifaa cha kupimia sukari, kifaa cha kupimia joto na nyinginezo.

Shughuli ya ugawaji wa vitu hivyo katika hospitali hizo uliudhuriwa na Mwenyekiti wa TPF Taifa, Sadick Godigodi na Katibu Mkuu wa taasisi hiyo Taifa, Fr. Meshack Chindundwa.

Mbali na viongozi hao wa kitaifa pia walikuwepo viongozi wa mkoa, viongozi wa wilaya zote za Jiji la Dar es salaam pamoja na viongozi wa Kata wa taasisi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi misaada hiyo kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Vijibweni, Dkt. Mtiba Nyahucho Mwenyekiti wa TPF, Sadick Godigodi amesema utaratibu huo utakuwa ukifanyika kila baada ya miezi sita na kwamba wanachama wameamua kujichanga ili kusaidia wagonjwa wenye mahitaji katika hospitali hizo.

Amesema hospitali nyingi zimekuwa zikilabiliwa na changamoto ya uhaba wa damu hivyo kitengo cha kutoa damu kwa ajili ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu ni jambo jema na kuitaka jamii kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu.
Amesema, kusaidia wagonjwa ni jukumu letu sote kama Jamii licha ya Serikali kubeba jukumu hilo hivyo jamii inapaswa kusaidia pia ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, aliwataka wanachama wa taasisi hiyo kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa waliopo katika hospitali mbalimbali hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanya jambo kubwa sana na Mungu atawabariki zaidi

Naye Mwenyekiti wa TPF Mkoa wa Dar es salaam, Sheikh Abdalha Hamad ametoa wito kwa watanzania kutoiachia serikali pekee bali nao wanawajibu wa kusaidia wagonjwa pale wanapoona kunahitaji la kufanya hivyo.

"Kwa sababu kuna hitaji kubwa la damu tumeona ni vyema kwa uchache Wetu tuchangie damu na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wagonjwa,"ameongeza Katibu wa TPF wilaya ya Kinondoni Sheikh Aboubakari Abdulswamad.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Vijibweni Dkt. Nyahucho amewashukuru viongozi na wanachama wa TPF kwa mchango wao kwani utasaidia kwa sehemu kubwa na kuwataka wajitoe zaidi na zaidi kwa kuwa wagonjwa waliopo Hospitalini ni watanzania hivyo wasibaguane kwa itikadi yoyote Ile.

Naye, Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto wachanga chini ya siku 28, Irene Balongo, amesema wanaishukuru TPF kwa kuchangia damu kwa kuwa utasaidia kupunguza vifo vya akina mama na kwamba wanachangamoto ya vipimo vya sukari na vipimo vya joto.

Post a Comment

0 Comments