TASAF kuongeza tabasamu kwa vijiji na mitaa yote nchini

Na Yusuph Mussa, Diramakini Blog

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Kipindi cha Pili utafika kwenye vijiji na mitaa yote Tanzania Bara, huku ukizifikia shehia zote kwenye Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuingiza kaya zote zinazoishi katika mazingira duni ziweze kutambuliwa, na zile zitakazokidhi vigezo zitaandikishwa kwenye daftari la walengwa wa TASAF, na hatimaye kuanza kupokea ruzuku na kuziwezesha kaya hizo kujikimu na kuanzisha miradi itakayowatoa kwenye hali duni.
Magembe Musika akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini Ladislaus Mwamanga. Ni kwenye kikao kazi cha uelewa juu ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli. (Picha na Yusuph Mussa).

Hayo yamesemwa Julai 6, 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini Ladislaus Mwamanga kwenye kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mfuko wa TASAF kilichowashirikisha madiwani, wakuu wa idara na vitengo na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli mkoani Tanga.

Kwenye hotuba yake iliyosomwa na Magembe Musika, Mwamanga alisema Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kinatekelezwa katika halmashauri 184 Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar, na kitazifikia kaya milioni 1,450,000 zenye watu milioni saba kote nchini, mkazo mkubwa ukiwa umewekwa katika kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye Mpango kufanya kazi ili kuongeza kipato.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli wakiwa kwenye picha ya pamoja na Magembe Musika (wa tatu kulia waliokaa) ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini Ladislaus Mwamanga. Ni kwenye kikao kazi cha uelewa juu ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli. Katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amiri Shehiza na wa kwanza kulia ni Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Bumbuli Christian Mauya. (Picha na Yusuph Mussa).

Aidha, Kipindi cha Pili kitahakikisha kwamba huduma za jamii zinaboreshwa na kuongezwa, nia ikiwa kuboresha huduma na kuendeleza rasilimali watoto hususani katika upatikanaji elimu na afya.

"Kipindi cha Kwanza cha Awamu hii ya Tatu ya TASAF hakikufika katika maeneo yote. Kuna vijiji na mitaa haikufikiwa, na maswali yalikuwa mengi kuhusu lini maeneo yaliyobaki yatafikiwa. Ni furaha yangu kuwajulisha kwamba maeneo yote ambayo hayakufikiwa katika Kipindi cha Kwanza muda wake umefika.

"Hivyo, katika Kipindi cha Pili tutafika kwenye vijiji na mitaa yote Tanzania Bara pamoja na shehia zote za Unguja na Pemba kwa Zanzibar. Kaya zote zinazoishi katika mazingira duni zitatambuliwa, na zile zitakazokidhi vigezo zitaandikishwa kwenye daftari la walengwa wa TASAF, na hatimaye kuanza kupokea ruzuku na kuziwezesha kaya hizo kujikimu na kuanzisha miradi itakayowatoa kwenye hali duni" alisema Mwamanga.
Wawezeshajii wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli wakiwa kwenye picha ya pamoja na Magembe Musika (wa tatu kulia waliokaa) ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini Ladislaus Mwamanga. Ni kwenye kikao kazi cha uelewa juu ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli. Katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amiri Shehiza na wa kwanza kulia ni Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Bumbuli Christian Mauya. (Picha na Yusuph Mussa). 

Mwamanga alisema Kipindi cha Pili kilianza kwa zoezi la uhakiki kwa kaya za walengwa wote, na kuondoa kaya zote za walengwa ambazo hazikuwa na vigezo ama walengwa hewa kama walivyofahamika. Na hiyo ni kutokana na malalamiko kutoka kwenye jamii kwamba ndani ya walengwa kuna watu ambao hawakuwa na vigezo, mfano kaya ambazo hazikuwa na maisha duni.

"Lakini pia kulikuwa na kaya za viongozi, lakini pia na watu ambao hawakuwa wakazi wa maeneo husika, au waliofariki. Ilibidi kuanza na kusafisha daftari letu la walengwa na kuondoa dhana iliyojengeka kwa jamii ya kuwemo walengwa hewa kwenye Mpango wa TASAF. Katika zoezi hilo, kaya ambazo hazikuwa na vigezo ziliondolewa kwenye orodha," alisema.
Kikao kazi cha uelewa juu ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli. (Picha na Yusuph Mussa).
Kikao kazi cha uelewa juu ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli. (Picha na Yusuph Mussa).

Awali, akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Amiri Shehiza aliwataka madiwani, wakuu wa idara, wakuu wa vitengo na wawezeshaji wa TASAF kuweza kushirikiana ili kufanikisha zoezi hilo, na hasa wawezeshaji ambao ni watumishi wa Serikali kwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na weledi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Protas Dibogo alisema ili zoezi la uhakiki wa walengwa wa Mpango kufanywa kwa weledi, Serikali iliamua kuchukua watumishi wa Serikali ambao watakuwa na maadili katika kusimamia zoezi hilo, na viapo vyao wanavyoapa ndiyo vinawafunga katika kuona hawamuonei mtu ama kufanya upendeleo.

Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Christian Mauya alisema halmashauri hiyo ina vijiji 83, ambapo vilivyokuwa kwenye Mpango ni 52, na sasa kwenye Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF, vijiji 31 vilivyokuwa vimebaki, vinakwenda kuingizwa humo, na kufanya vijiji vyote 83 vya Bumbuli kuwa kwenye mpango

Post a Comment

0 Comments