Wananchi washauriwa kukabiliana na ugonjwa wa shinikizo la damu

Na Dorcas David

Wananchi wameshauriwa kubadili mtindo wa maisha ili kukabiliana na ugonjwa wa shinikizo la damu ambao unawakabili watu wazima wenye umri kuanzia miaka 40.
Hayo yamesemwa na Dkt Gerald Kalinga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati akitoa ushauri kwa wananchi mbalimbali waliotembelea Banda la Muhimbili (Upanga& Mloganzila) liliolopo katika viwanja vya Sabasaba.

Dkt. Kalinga amesema kutofanya mazoezi na kutozingatia taratibu za lishe kunasababisha mtu kuwa na uzito uliopitiliza hivyo kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa shinikizo la damu.

“Ili kuepuka shinikizo la damu tunatakiwa kuzingatia kwa kiasi kikubwa kufanya mazoezi na kula mlo kamili ambao umejengwa na makundi matano ya chakula ambayo ni vyakula vya mafuta, wanga, protini, vitamin na madini,” amesema Dkt Kalinga.

Aidha, amesema ugonjwa wa shinikizo la damu unaweza kusababishwa na sababu nyinenezo ikiwemo ugonjwa wa figo,ugonjwa wa kisukari.

Naye Afisa Lishe Bi. Theresia Raymond ametaja vyakula vyenye mafuta kuwa ni mbegu za mafuta, mafuta ya kupikia na matunda kama maparachichi na kwa upande wa vyakula vya wanga ni jamii ya nafaka mizizi kama viazi na mihogo, ndizi na baadhi ya mbogamboga.

Kwa upande wa protini ni vyakula jamii ya nyama aina zote, mazao ya wanyama kama maziwa na mayai, ndege, jamii ya kunde na wadudu wanaoliwa kama senene na kumbikumbi. Na vitamin na madini ni pamoja na mboga za majani na matunda.

Kwa upande wake mzee Wilfred Miigo aliyeanza kuugua ugonjwa wa shinikizo la damu tangu mwaka 1996 amewashauri wale ambao tayari wana ugonjwa huo kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kwani tangu ameanza kutumia dawa afya yake imeimarika anaendelea na majukumu yake kama kawaida.

Mzee Miigo amewapongeza wataalamu wa Hospitali ya Muhimbili kwa huduma nzuri wanazotoa, amesema mtu unahudumiwa na kujisikia vizuri sana na kusahau kama mtu unaumwa.

“Nawapongeza sana, huduma zenu ni nzuri, nimehudumiwa mara kadhaa katika hospitali zenu kule Muhimbili Upanga na Mloganzila mambo safi,’’ amesema mzee Miigo.

Wananchi mbalimbali wameendelea kujitokeza kwenye Banda la Muhimbili kupata huduma ya meno, macho, huduma, za dharura, ushauri kuhusu lishe, magonjwa ya mfumo wa vyakula na elimu kuhusu magonjwa ya figo.

Post a Comment

0 Comments