Afisa Lishe awapa mwanga akina mama wanaonyonyesha kipindi hiki cha Corona

Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog

IKIWA Taifa na Dunia kwa ujumla inaendelea kupambana na Ugonjwa wa CORONA, mama wanaonyonyesha wametakiwa kuona umuhimu na kuzingatia kanuni zinazoshauriwa katika unyonyeshaji wa watoto wachanga pamoja na kuchukua tahadhari za kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.
Unyonyeshaji husaidia kuimarika kwa kingamwili ya mtoto kuwa na ukuaji mzuri kimwili na kiakili huku takwimu zikionyesha Tanzania kuwa na asilimia 58 ya watoto chini ya miezi sita wananyonya maziwa ya mama.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Tafiti Mwandamizi Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania,Ruth Mkopi wakati alipokuwa akizungumza na DIRAMAKINI BLOG juu ya namna mama anayenyonyesha anavyotakiwa kumlinda mtoto wake katika kipindi hiki Taifa linavyoendelea kupambana na Ugonjwa wa CORONA.

Mkopi amesema kuwa, pamoja na kuibuka kwa ugonjwa wa COVID- 19 unyonyeshaji wa maziwa ya mama bado una manufaa makubwa kwa afya na ukuaji wa mtoto na kuimarisha mfumo wa kingamwili ya mtoto.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani mpaka sasa hakuna ushahidi wa kitafiti unaoeleza uwepo wa maambukizi ya virusi vya corona toka kwa mama kwenda kwa mtoto kipindi cha ujauzito au kupitia maziwa ya mama wakati wa unyonyeshaji.

"Nipende kuwasihi mama hasa wanaonyonyesha watoto wadogo katika kipindi hiki tunachoendelea kujikinga na gonjwa la Corona, naomba muendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu ili muweze kuwalinda watoto wenu,"amesema Mkopi.

Aidha, katika hatua nyingine Mkopi amedai kuwa, wazazi wanapaswa kulinda afya za watoto chini ya miezi sita kwa kuepuka kuwapa maziwa na makopo yanayouzwa madukani kwa uzushi kuwa yanaondoa maradhi kwa mtoto jambo ambalo sio sahihi.

"Kuna baadhi ya makampuni yanayotengeneza maziwa na vyakula vya watoto wachanga na wadogo yanatumia masoko ya kidijitali kutangaza bidhaa zao kwa wanawake, hivyo kukiuka utekelezaji wa kanuni za kitaifa. Jamii itambue kuwa hayo maziwa sio mazuri kwa watoto wachanga, hivyo katika kipindi hiki cha CORONA tuwe makini sana,"amesema.

"Tanzania ni mojawapo ya nchi 25 zinazotekeleza kanuni inayosimamia uuzaji na usambazaji wa maziwa mbadala na vyakula vya watoto wachanga na wadogo kikamilifu,"amesema Mkopi.

DIRAMAKINI BLOG  ikaongea na baadhi ya mama wanaonyonyesha,Amina Adamu mkazi wa Nkuhungu,Avelina Moses mkazi wa Makulu jijini hapa wamesema kuwa tangu Serikali itangaze kuwa ugonjwa wa Corona unaweza kuwapata hata watoto wadogo wamekuwa na wasiwasi wakidhani wanaweza kupata maambukizi kutoka kwa mama zao endapo watapatwa na ugonjwa huo na kuwanyonyosha.
Amina Adamu amesema kuwa, tayari amepatiwa chanjo ya COVID-19 ambapo alihofia afya ya mtoto wake anayemnyonyesha akidhani kwamba itaenda kumdhuru mtoto wake.

Alida Mkebezi mkazi wa Kikuyu jijini Dodoma ni mama mwenye mtoto wa miezi sita amesema kuwa, ktika kipindi hiki cha janga la CORONA ambalo linawafikia Hadi watoto, Serikali ina kila sababu ya kuendelea Kutoa elimu jinsi gani watoto wataepukana na maambukizi hayo kwani wengi hawana amani na wanaogopa kwenda kuchanja kwa sababu ya hofu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news