Askofu wa Kanisa la TAG afariki baada ya maumivu makali ya mwili

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) limepata msiba mkubwa baada ya kuondokewa na Mwasisi na Askofu wa Kwanza wa kanisa hilo mkoani Tabora ambaye pia ni Askofu wa Kwanza wa TAG Kanda ya Magharibi, Mzee William Lusito.

Askofu William Lusito mwenye umri wa zaidi ya miaka 80, amefariki dunia juzi mchana mjini hapa ambapo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mwili kwa muda mrefu.

Akizungumzia msiba huo Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG-Kitete Christian Centre (KCC) lililoanzishwa na marehemu Askofu Lusito, Rev. Paul Meivukie amesema, kanisa limepata msiba mkubwa sana kwa kuondokewa na kiongozi huyo.

Amesema, katika utumishi wake marehemu alifanya kazi kubwa ya kuhubiri injili na kupanda makanisa mengi katika Mkoa huo na Mikoa yote ya Kanda ya Magharibi na aliaminiwa sana kwa utumishi wake usio na mashaka mbele za Mungu.

Amebainisha kuwa, marehemu Askofu Lusito ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kiroho Mkoani hapa kwa miaka mingi ametoa mchango mkubwa sana kwa kanisa la TAG na makanisa mengine hapa nchini.

"Tumepoteza Mzee wetu, Baba yetu na Mtumishi wa Mungu, tutamwenzi kwa kufanyia kazi yale yote aliyokuwa akituambia, jumapili iliyopita aliomba ahubiri lakini akashindwa, alikuwa hajisikii vizuri, ningefurahi kama angehubiri ili atuage,"amesema.

Meivukie amebainisha kuwa, mazishi ya marehemu Askofu Lusito yataongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG hapa nchini Dkt Barnabas Mtokambali na yatafanyika kesho katika eneo la kanisa la KCC mjini Tabora.

Mzee Kiongozi wa kanisa hilo, Dkt.Frank Mtimbwa ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi alisema Askofu Lusito mbali ya kuwa mwaasisi wa kanisa la KCC, pia ana mchango mkubwa sana katika kuinua makanisa ya kipentekoste.

Amesema, marehemu alikuwa mtu wa watu na alimtumikia Mungu kwa moyo wa dhati, alianzisha makanisa mengi sana na kila alikokwenda kuhubiri alianzisha kanisa na amezaa wachungaji wengi.

Naye Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo Shedrack Herman alisema marehemu alikuwa karibu sana na Mungu na hata kipindi alichokuwa anaumwa alikuwa anatumia muda wake mwingi kumwomba Mungu.

"Tutamkumbuka sana Mzee wetu kwani alikuwa msaada mkubwa kwa wachungaji wa makanisa ya kipentekoste, ameacha kitabu cha historia ya maisha yake ya utumishi, ambacho kilikuwa katika hatua za mwisho kukamilika," amesema.

Akiongea kwa niaba ya waumini wa kanisa la KCC, Novatus Kifumbu ambaye pia ni Shemasi wa kanisani hilo alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo kutokana na heshima kubwa aliyokuwa akipewa marehemu kanisa hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news