Mbunge Askofu Gwajima, Jerry Silaa waondolewa kwenye kamati

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Askofu Josephat Gwajima ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kawe na Jerry Silaa wa Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge wameondolewa kwenye kamati hiyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Agosti 24,2021 hadi itakapoamuliwa vinginevyo Bungeni jijini Dodoma.
Askofu Josephat Gwajima na Jerry Silaa wameitwa mbele ya kamati hiyo wakituhumiwa kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

Kamati hiyo ina jumla ya wajumbe 24 wakiwamo Gwajima na Silaa na sasa imebaki na wajumbe 22 baada ya hatua hiyo.

Mheshimiwa Askofu Gwajima alianza kuhojiwa Agosti 23,221 na kamati hiyo kwa zaidi ya saa mbili na Agosti 25,2021 ataendelea kuhojiwa.

Kwa upande wa Mheshimiwa Silaa atahojiwa leo mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Emmanuel Mwakasaka.

Mwakasaka amesema, unapotuhumiwa mara nyingi, wewe ndio mshtakiwa.

"Hivyo zipo taratibu zinafuata. Kama wewe ni mtuhumiwa huwezi kuwa hakimu kwenye kesi yako mwenyewe,”amesema Mheshimiwa Mwakasaka huku akiongeza kuwa, tayari wajumbe hao wameondolewa katika kamati.

Jana baada ya mahojiano hayo kufanyika Mwenyekiti wa Kamati, Emmanuel Mwakasaka amesema wamemaliza kusikiza shauri la Askofu Gwajima ambapo ametoa ushirikiano.

“Askofu Gwajima ametoa ushirikiano wa kutosha, bado suala hili linaendelea kazi yetu kama kamati ni kuchunguza Mbunge anayekiuka maadili na kanuni za bunge tumemruhusu aende, lakini shauri lake bado linaendelea,"amesema.

Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa hawawezi kusema kama akikutwa na hatia atachukulia hatua gani au kupewa adhabu gani kwa kuwa zipo nyingi na mwenye kazi hiyo ni Spika wa Bunge peke yake, Mheshimiwa Job Ndugai.

MUHIMU


UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE

Post a Comment

0 Comments