Muungano wa EREA wajitambulisha kwa Waziri wa Nishati

Na Zuena Msuya, Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na Muungano wa Taasisi za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita (6) za Afrika Mashariki (EREA) mara tu taasisi hiyo itakapokamilisha taratibu zinazotakiwa.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na Katibu Mtendaji wa Muungano wa Taasisi za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita (6) za Afrika Mashariki (EREA), Dkt. Geoffrey Mabea,(kulia) alipofika ofisini kwa waziri huyo Jijini Dodoma, Agosti 17, 2021, kutambulisha taasisi hiyo.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa EREA,Dkt. Geoffrey Mabea na ujumbe wake, walipofika ofisini kwa Waziri huyo jijini Dodoma, Agosti 17, 2021, kujitambulisha, kwa lengo la kueleza majukumu yao juu ya muungano huo na namna inavyofanya kazi kwa nchi husika.

Dkt. Kalemani alisema kuwa Wizara ya Nishati, iko tayari kushirikiana na EREA katika kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya nchi za Afrika Mashariki, kwakuwa nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha aliitaka taasisi hiyo kukamilisha rasimu ya Mkataba wa utekelezaji wa majukumu yake ili isambazwe kwa nchi husika ili kila moja iweze kutoa maoni yake.

Sambasamba hilo alizishukuru taasisi za kifedha hasa Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kufadhili wa uundwaji wa Taasisi hiyo na kuwa bega kwa beka katika kukuza Sekta ya Nishati nchini.
Kamishna wa Umeme na Nishati jadidifu Wizara ya Nishati, Edward Ishengoma (kushoto), Kamishna wa Mafuta na Gesi, Adam Zuberi (kulia), Mhandisi Shukrani Rugaimukamu Wizara ya Nishati (pili kushoto) na Mhasibu Mkuu wa (EREA) Augustino Massawe wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo picha) wakati akizungumza na ujumbe wa Muungano wa Taasisi za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita (6) za Afrika Mashariki (EREA).

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa EREA, Dkt. Geoffrey Mabea, aliipongeza Tanzania kupitia Wizara ya Nishati kwa kuwa nchi ya tatu (3) Afrika katika uthibiti wa masuala ya nishati.

Vilevile alieleza kuwa taasisi hiyo ina malengo makubwa matatu, moja likiwa ni kuwezesha muunganiko wa kisera katika masuala ya nishati kwa nchi wanachama katika kazi za udhibiti wa bei za mafuta na umeme.

Pia kufanya tafiti za kisera hususani katika sekta ya nishati na kuwezesha ushirikishwaji wa taarifa kwa nchi za Afrika Mashariki na kujenga uwezo kwa Taasisi za Udhibiti kwa nchi wanachama pamoja na washirika wote katika sekta ya nishati.

Dkt. Mabea alitaja nchi wanachama katika taasisi hiyo kuwa ni Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Sudani Kusini ambapo makao makuu ya tasisi hiyo yapo mjini Arusha, na kwamba ilianzishwa rasmi mwaka 2009.

Hata hivyo alieleza kuwa, tayari imeandaliwa rasimu ya Mkataba wa Makubaliano ambao utasambazwa kwa nchi wanachama ili waweze kutoa maoni, na Mkataba huo ukikamilika utapelekwa kwa kila nchi wanachama ili uweze kusainiwa.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akimsikiliza Katibu Mtendaji wa Muungano wa Taasisi za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita (6) za Afrika Mashariki (EREA), Dkt. Geoffrey Mabea( wa pili kulia) alpofika ofisini kwa waziri kutambulisha taasisi hiyo, wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa huduma za Nishati na Maji(EWURA), Mhandisi Godfrey Chibulunje.

Lengo la mkataba huo ni kusaidia kuridhia ujenzi wa Chuo cha Udhibiti kinachotarajiwa kujengwa Nchini Tanzania katika Jiji la Arusha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news