Mwanamke mbaroni kwa kutuhumiwa kumuua mumewe kwa shoka

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mkazi wa Kijiji cha Garanja, Kata ya Tlawi, Wilayani Mbulu, Mkoani Manyara, Maria Suruhu (56) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga kichwani na shoka mume wake, Lego Kerehemi (54).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) Marrison Mwakyoma amesema tukio hilo limetokea kwenye Kata ya Tlawi.

Kamanda Mwakyoma amesema  chanzo cha kifo ni ugomvi wa ndani baada ya mwanamke huyo kuulizwa alipochelewa baada ya wote kutoka kunywa pombe kilabuni.

Amesema, mume na mke walienda kilabuni kunywa pombe na walipomaliza waliamua kurudi nyumbani huku wakiongozana wawili barabarani.

"Baadaye waliachana njiani kila mmoja akafuata njia yake ila kufika nyumbani mume akawahi kufika na mke akachelewa kidogo," amesema Kamanda Mwakyoma.

Amesema, mume akamuuliza mkewe kwa nini amechelewa kurudi muda wote huo na ndipo akaanza kumpiga kwa kosa hilo.

"Wakati wakiendelea kupigana mke alichukua shoka na kumpiga nalo kichwani mume wake na kusababisha kifo chake papo hapo," amesema Kamanda Mwakyoma.

Amesema, mwanamke huyo Suruhu anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji hayo na anatarakiwa kufikishwa mahakamani pindi uchunguzi ukikamilika.

Mkazi wa eneo hilo, Julius Slaa amesema kwa sasa watoto wa familia hiyo wamepata pigo kubwa kutokana na tukio hilo kwani ni sawa na kuwapoteza wazazi wote wawili.

"Baba amefariki dunia kwa kuuawa na mama ambaye hivi sasa yupo mahabusu kutokana na ulevi wao hatima ya watoto itakuwa mbaya," amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news