RC Dkt.Sengati aizuia Buzwagi kuhamisha mali mgodini, kuunda tume uchunguzi wa miradi

Na Anthony Ishengoma,Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Philemon Sengati ameutaka mgodi wa Buzwagi ambao tayari umesimamisha shughuli zake kutohamisha mali zozote kutoka ndani ya mgodi wala kufungua mitambo ya uchenjuaji madini mpaka Kamati ya Taifa ya Ufungaji Mgodi itakapojiridhisha na kufikia muafaka.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akiongoza wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Ufungaji Mgodi katika majadiliano ya ufungaji mgodi huo katika ofisi za mgodi huo Buzwagi Kahama mkoani Shinyanga.


Dkt.Sengati aliiambia Menejimenti ya Mgodi mbele ya wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Ufungaji Mgodi wa Buzwagi kuwa, Kamati hiyo inazingatia uwepo wa muafaka mzuri ambao unazingatia maslahi mapana ya serikali na kutaka vyombo vya ulinzi kusimamia zoezi hilo mpaka kamati na mgodi watakapofikia muafaka.

Dkt. Sengati alisema hayo wakati yeye na Kamati ya Taifa ya Kufunga mgodi walipotembelea miradi ambayo mgodi huo umeahidi kutekeleza kama faida ya uwepo mgodi huo kwa jamii na kubaini miradi hiyo ni miradi bubu ambayo ipo kuwadaa wananchi na serikali.

‘’Nawataka kutojikita katika kuhamisha mali za mgodi kwa sababu suala hilo lipo kisheria,"amesema na kuonya kuwa kama watakiuka agizo lake serikali iko macho na watachukuliwa hatua.

Katika hatua nyingine Dkt.Sengati amesema, ataunda tume kuchunguza matumizi ya fedha za miradi iliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo inaonekana na miradi isiyokidhi thamani ya fedha iliyotajwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa Kamati kuwa Mgodi umetenga dola milioni 1.1 kwa ajili ya mradi wa Kilimo lakini uwekezaji katika mradi huo hauendani na thamani ya fedha hiyo.
Meneja wa Mgodi wa Buzwagi, Bi. Rebeka Stivini akiwasilisha mada kwa Kamati ya Taifa ya Ufungaji mgodi mapema jana wakati wa majadiliano ya ufungaji mgodi huo katika ofisi za mgodi huo Buzwagi Kahama mkoani Shinyanga.


Suala hilo likamsukuma Dkt. Sengati kuunda Tume ya kuchunguza thamani ya fedha iliyotolewa kwa miradi yote iliyo chini ya mradi huo ikiwemo mradi wa ufugaji nyuki na Skimu ya Umwagiliaji na tume hiyo itaundwa na wataalam wa fedha, Takukuru na vyombo vya usalama kwa lengo la kujiridhisha na kama itabainika kuna ubadhirifu hatua za kisheria zitachukuliwa.
Mradi huo awali uliozinduliwa na Kiongozi wa mbio za Mwenge mwaka huu, Luteni Josephine Mwambashi ambao baada ya Kamati kuukagua amegundua hauendani na kiasi cha rasilimali fedha zilichotolewa na mgodi huo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Bw. Anderson Nsumba aliiambia kamati hiyo kuwa mgodi ulikataa kufuata mpango ambao Halmashauri iliwasilisha kwao baada ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusanifu mradi huo na kupendekeza kuwa utekelezaji wake ungegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni kumi, lakini Buzwagi wanataka kutekeleza mradi huO kwa kiasi cha milioni 700 na kulingana na ukubwa wa eneo fedha hizo haziwezi kuleta tija.

Kamati hiyo pia ilitembelea uwanja wa ndege wa Buzwagi ambao kwa kipindi kirefu umekuwa ukitumiwa na Mgodi ambao kwa sasa uko katika hali mbaya kutokana na kuchakaa hali iliyomsukuma Dkt. Sengati kuangazia suala la uwanja huo.

Dkt. Sengati akautaja uwanja huo kuwa wa umuhimu kwa uchumi wa Kahama hivyo ni vyema Manejimenti ya Mgodi ikashauriwa kuhusu matengenezo yake na kuongeza kuwa ingekuwa vyema wakawekeza katika miradi yenye tija badala ya kuwekeza katika miradi mingi midogo midogo ambayo haina maana kwa jamii.

Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Ufungaji Mgodi wakikagua Skimu ya Umwagiliaji ambayo inatarajiwa kufadhiliwa na Mgodi wa Buzwagi iliyoko nje kidogo ya Manispaa ya Kahama.

Meneja wa Mgodi huo Bi.Rebeka Stivin aliiambia kamati hiyo kuwa, uwanja wa ndege hauko tena mikononi mwao kwani tayari wamekabidhi mamlaka za viwanja vya ndege nchini, lakini kamati hiyo ilipendekeza ukarabati huo ni bora ukakarabatiwa na mgodi kwa kuwa taratibu za kufunga mgodi bado zinaendelea chini ya kamati hiyo.

Aidha, mgodi wa Buzwagi unataka kukarabati tu jengo la abiria wakati njia ya kurushia ndege ikiwa imejaa mashimo na kwa mujibu wa Manispaa ya Kahama gharama za ukarabati uwanja huo ni takriban bilioni 4.

Naye Bi. Sundi Malomo kutoka Tume ya Taifa ya Madini alisema kuwa, sheria iko wazi kwamba mwekezaji anapotaka kutoka lazima aangalie namna ya kuilinda jamii namna ya kuishi akiutaka uongozi wa Mgodi kuangalia upya bajeti yao ili mradi uweze kutekelezeka.

Kamati hiyo imekuwa katika Majadiliano ya Siku tatu na Utawala wa Mgodi huo na Kamati hiyo imeutaka Utawala wa Mgodi kuheshimu makubaliano yatokanayo na Majadiliano hayo ikiwemo yale ya vikao vya awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news