WANAFUNZI WATANO WAFARIKI KWA AJALI,RC PWANI ASHIRIKI MAZISHI

Na Rotary Haule, Chalinze

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge leo Agosti 7,2021 ameshiriki kwenye mazishi ya watoto watano waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha Pikipiki na gari ya mizigo aina ya Fuso iliyotokea eneo la Kata ya Kimange Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge akizungumza katika mazishi ya wanafunzi watano waliofariki katika ajili ya gari iliyotokea Agosti 6, mwaka huu katika eneo la Kimange Chalinze Mkoani Pwani. (Picha na Rotary Haule).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kuwa, ajali hiyo imetokea Agosti 6, 2021 majira ya saa 1 jioni ambapo gari aina Mitusubish Fuso yenye namba za usajili T 198 CWN ikitokea Dar es salaam kwenda Arusha lilimgonga mwendesha Pikipiki na kusababisha vifo vya wanafunzi wanne papo hapo na mmoja kufariki akipatiwa matibabu Hospital ya Jeshi Kihangaiko.

Kamanda Nyigesa amesema, wanafunzi hao watano wa Kimange Sekondari walikuwa wamepakiana kwenye Pikipiki moja wakitokea Kimange kuelekea Mbwewe na kusema wanafunzi hao walikuwa wakitokea michezoni shule jirani ya Kwamakocho Sekondari.

Nyigesa aliwataja wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Laya Masudi (16) mwanafunzi wa Kimange Sekondari Kidato cha tatu, Furaha Athumani (16) Mwanafunzi Kimange Sekondari Kidato cha tatu, Athumani Bushiri (15) Mwanafunzi Kimange Sekondari Kidato cha Kwanza, Amina Msomba (15) Mwanafunzi Kimange Sekondari Kidato cha Kwanza na Athumani Mchafu (17) Mwanafunzi Kidato cha tatu.

Aidha,Kamanda huyo ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari ambaye alikuwa mwendokasi uliosababisha kushindwa kumudu gari hilo na kupelekea kumgonga mwendesha Pikipiki akiyekuwa mbele yake.

Nyigesa amesema, mpaka sasa tayari Jeshi lake limefanikiwa kumshikilia dereva wa gari hilo kwa ajili ya hatua za kisheria .

RC Kunenge ametoa pole kwa familia na Wananchi wa Kata hiyo kwa msiba mkubwa ambao wamehupata huku akisema Serikali ipo pamoja na familia iliyopatwa na msiba huo katika kipindi hiki kigumu.

"Kubwa zaidi kwetu ilikuwa ni kuja kushiriki nanyi katika msiba huu mzito na tumekuja na sadaka ndogo kwa ajili ya kufariji familia hizi,"amesema Kunenge.

"Yaliyotokea yametokea, niwaombe tuzingatia matumizi ya vyombo vya moto lakini sisi kwa upande wa Serikali tunaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi,"ameongeza Kunenge.

Hata hivyo,Kunenge amesema dereva wa gari hilo atachukuliwa hatua za kisheria mara moja ikiwa ni pamoja na kupelekwa Mahakamani pale taratibu zitakapokamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news