ASKOFU LUTUBIJA WA TMRC ASTAAFU, AWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA AMANI NA KUIOMBEA NCHI WAKATI WOTE

Na Fresha Kinasa, Mara

Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) nchini, Jacob Lutubija amestaafu rasmi baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 20 katika nafasi hiyo, ambapo amewataka Waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa wakati wote na kudumu katika upendo na umoja.
Askofu Mkuu wa Kanisa la TMRC nchini kwa sasa, Julius Kisandu kushoto akimkabidhi cheti cha heshima Askofu mstaafu wa manisa hilo, Jacob Lutubija baada ya kulitumikia kanisa kwa kipindi cha miaka 20 akiwa Askofu Mkuu.

Hafla ya kumuaga Askofu Lutubija ilifanyika Jumapili Septemba 26, 2021katika Kanisa la TMRC Kigera lililopo Manispaa ya Musoma na kuhudhuriwa na Maaskofu wa madhehebu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mara pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa la TMRC kutoka Makao makuu jijini Mwanza.

Akisoma risala ya utumishi wa Askofu Lutubija, Katibu Mkuu wa Kanisa la TMRC Tanzania, Askofu Joseph Butondo alisema kuwa Askofu Lutubija amekuwa kiongozi bora ndani ya kanisa hilo ambapo tangu mwaka 1972 alikuwa mchungaji na alihudumu katika Wilaya ya Ukerewe, Geita na baadaye kuhamia Mkoa wa Mara mwaka 1999 ambapo alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa TMRC nchini hadi mwaka 2019. na hivyo kutimiza miaka 20 ya Uaskofu wa kanisa hilo.

Alisema katika utumishi wake, Askofu Lutubija ameweza kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu na ushujaa mkubwa ambapo kabla ya kuchaguliwa kuwa Askofu kanisa hilo lilikuwa katika mikoa sita pekee nchini. Lakini kwa kipindi chake cha utumishi limeweza kufika mikoa mbalimbali hapa nchini sambamba na kuwezesha ujenzi wa kituo cha Afya cha ''Urafiki Health Center''kilichopo Igoma Mkoa wa Mwanza kinachoendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Askofu Jacob Lutubija wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church ambaye amestaafu baada ya kuhudumu kwa muda wa miaka 20.
Askofu Jacob Lutubija akipokea cheti kutoka kwa Katibu Mkuu wa Kanisa la TMRC nchini, Askofu Joseph Butondo ambacho kilitolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mh. Ally Happy ikiwa ni ishara ya kutambua ushirikiano wake na kanisa hilo.
Askofu Butondo aliongeza kuwa, Kanisa hilo litaendelea kuthamini kwa dhati kazi kubwa iliyofanywa na Askofu Lutubija ikiwemo kuokoa roho za watu kutoka dhambini, kuimarisha umoja, maadili na kushirikiana vyema na Serikali katika kuhubiri amani, umoja na kuhamasisha uwajibikaji kwa manufaa ya Wananchi. Na pia akawahimiza Watumishi wengine ndani ya Kanisa hilo kufuata nyayo zake.

Kwa upande wake Askofu Jacob Lutubija ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya amani ya Mkoa wa Mara alisema kuwa, Mbali na kustaafu katika nafasi ya Uaskofu ndani ya Kanisa hilo bado ataendelea kushirikiana na Viongozi wa kanisa hilo kwa moyo wa dhati ikiwemo kuhudumu katika Kanisa la TMRC Kigera Manispaa ya Musoma na kutoa mawazo na Ushauri chanya utakaozidi kusukuma mbele kazi ya Mungu.

Pia, Askofu Lutubija aliwaomba Viongozi wa dini na Watanzania wote kuendelea kuliombea taifa na Viongozi wote wa Serikali kusudi Mungu awajalie hekima, uadilifu na maarifa yatakayokuwa chachu ya kuwaletea maendeleo wananchi huku pia akisisitiza amani iliyopo nchini izidi kutunzwa kama mboni ya jicho na watu wote kwani ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Askofu Jacob Lutubija akiwa na mkewe wakati wa hafla ya kuagwa baada ya kulitumikia Kanisa hilo katika nafasi ya Uaskofu kwa kipindi cha miaka 20.
Viongozi mbalimbali na Maaskofu wakiwa katika hafla ya kumuaga Askofu Jacob Lutubija wa kanisa la TMRC baada ya kustaafu rasmi katika nafasi hiyo ambapo ameitumikia kwa muda wa miaka 20.
Aliwaomba pia viongozi wa dini kushiriki kikamilifu kuwahimiza waumini wao kushiriki katika zoezi la Sensa muda utakapofika kwani jambo hilo alisema ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa wananchi. Huku pia akiwaomba Watanzania kuendelea kupendana, kuthaminiana na kusaidiana kama ambavyo Neno la Mungu linaagiza.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church kwa sasa, Julius Magaka Kisandu aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuheshimu Uhuru wa kuabudu na pia akawaomba viongozi wa dini zote kuzidi kutumia Uhuru huo vyema hususan kuhubiri umoja, amani na upendo kama ambavyo Kristo akifanya.
Askofu Jacob Lutubija katikati na kulia kwake Askofu Mkuu wa Sasa wa Kanisa hilo la TMRC Julius Kisandu wakiwa wameshika kalenda baada ya Kupewa zawadi na waumini wa Kanisa hilo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la TMRC nchini kwa Sasa, Julius Kisandu.
Askofu Kisandu pia alipongeza hatua ya Serikali ya kusikia kilio cha Wananchi kuhusu masuala ya tozo ambapo alisema kuwa hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kusikia kilio hicho na kufanya marekebisho katika tozo hizo imewapa ahueni Wananchi tofauti na awali. Akasistiza kuwa Kanisa litaendelea kuunga mkono Juhudi za serikali zinazofanywa kwa ajili ya Maendeleo ya Watanzania.

Neema Mathias ni ambaye ni mkazi wa Kata ya Kigera Manispaa ya Musoma ameeleza DIRAMAKINI Blog kuwa, Askofu Lutubija amekuwa kiongozi bora katika kusaidia jamii hususani wahitaji bila kujali dini zao sambamba na kuhimiza maadili mema kwa vijana na jamii.

Post a Comment

0 Comments