Dkt.Mabula atoa maagizo mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na Magereza mjini Kondoa

Na Munir Shemweta, KONDOA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula ameiagiza Halmashauri ya Mji wa Kondoa kushughulikia mgogoro wa ardhi kati ya Gereza la King’ang’a na wananchi katika halmashauri hiyo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula akizungumza katika kikao na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo Septemba 21, 2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma.

Dkt.Mabula ametoa maelekezo hayo leo Septemba 21,2021 alipokutana na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya na mji wa Kondoa akiwa katika mwanzo wa ziara yake ya siku tano katika mkoa wa Dodoma

Amesema, suala la migogoro ya mipaka linapaswa kushughulikiwa na halmashauri husika na juhudi za makusudi zisipochukuliwa basi migogoro ya ardhi haiwezi kuisha katika halmashauri.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, mgogoro unaoendelea sasa iwapo pande zinazopingana zingekaa pamoja na kushughulikia suala hilo ungekuwa umekwisha kwa kuwa wananchi walisharidhia kuachia sehemu ya eneo kwa shughuli za magereza.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa,Dkt. Khamis Mkanachi akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo Septemba 21, 2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma.

Katika kuharakisha utatuzi wa mgogoro huo, Naibu Waziri wa Ardhi alimuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma,Thadei Kabonge kupeleka wataalamu wa upimaji eneo hilo ili kuainisha mipaka na utekelezaji huo ufanyike haraka.

“Naelekeza halmashauri husika kukutanisha pande zote na kuangalia nyaraka za umiliki na utekelezaji wake ufanyike mapema ili kuondoa mgogoro huo,”amesema Dkt. Mabula.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameielekeza pia halmashauri ya Mji wa Kondoa kuhakikisha inawapatia viwanja takribani wananchi 200 katika eneo la Bicha ambapo halmashauri ilishachukua fedha kwa ahadi ya kuwapatia viwanja, lakini ilishindwa kutekeleza.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi, Thadei Kabonge akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo Septemba 21, 2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma.

“Halmashauri ya mji wa Kondoa mfikirie namna ya 'kusolve' (kutatua) huu mgogoro wa wananchi ambao mmeshachukua fedha kwa ajili ya kuwapatia viwanja na hapa ofisi ya Kamishna mkoa wa Dodoma katika wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba iende kupima viwanja kwa ajili ya kuwapatia wananchi,” amesema Naibu Waziri wa Ardhi.
Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, Ally Makoa akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo Septemba 21, 2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma. (Picha zote na Hassan Mabuye-WANMM).

Awali Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini mkoani Dodoma, Ally Makoa alimueleza Dkt.Mabula kuwa changamoto kubwa katika jimbo lake ni mgogoro kati ya wananchi na jeshi la Magereza, mgogoro wa eneo la hifadhi pamoja na ule mgogoro wa wananchi walinaotaka kupatiwa viwanja.

Alisema, migogoro hiyo ikitatuliwa basi katika mji huo wa Kondoa hautakuwa na migogoro ya asili na itakayoibuka ni ile itakayosababishwa na watu.

Post a Comment

0 Comments