NHC YAJA NA MKAKATI MKUBWA WA KUKARABATI NYUMBA ZAKE

Na Munir Shemweta, KONDOA

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limesema limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake katika maeneo mbalimbali nchini ili ziwe katika ubora.
Meneja wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya akizungumza katika kikao kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma leo Septemba 21,2021 akiwa katika ziara ya siku tano mkoani Dodoma. (PICHA NA HASSAN MABUYE- WIZARA YA ARDHI).

Hayo yamebainishwa leo Septemba 21, 2021 wilayani Kondoa mkoani Dodoma na Meneja wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo.

“Shirika letu la NHC lilianzishwa mwaka 1962 na sasa tumeanza kuzifanyia ukarabati nyumba zetu katika maeneo mbalimbali zikiwemo zile za Dar es Salaam ambapo kuna asilimia 60 ya nyumba zote za shirika,"amesema Saguya.

Kwa mujibu wa Saguya, NHC ina takribani nyumba 18,000 nchi nzima zinazotumika kwa shughuli za biashara na makazi na ukarabati unaofanyika utasaidia nyumba hizo kuwa na ubora na muonekano mzuri wa kuvutia.

Hata hivyo, Meneja huyo wa Kitengo cha Habari na Uhusiano NHC ameongeza kuwa, pamoja na ukarabati wa nyumba zake unaoendelea shirika la NHC linadai takribani shilingi bilioni 26 kutoka kwa wapangaji wake na kuwataka wote wanaodaiwa kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili fedha hizo zitumike kuendesha miradi mingine ya shirika.

Saguya amebainisha kwa kusema, Shirika la Nyumba la Taifa, kwa sasa linaendelea na miradi yake ya ujenzi wa nyumba za kuuza na zile za kupangisha kwenye mkoa wa Dodoma na sasa linakamilisha mradi wa nyumba 300 eneo la Iyumbu na nyumba 100 eneo la Chamwino.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula alisema, katika kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kabla kuanza ujenzi shirika la nyumba linatakiwa kufanya mawasiliano na taasisi kama TARURA, Maji na TANESCO ili kusaidia uwezeshaji miundo mbinu katika eneo la mradi.

Amebainisha kuwa, NHC kwa sasa inajenga nyumba kwa wanaohitaji kulingana na chaguo la mteja hivyo ni fursa kwa halmashauri kulitumia shirika katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba.

Post a Comment

0 Comments