Fedha za umma zaondoka na vigogo wawili

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Omary Mgumba ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe amewasimamisha kazi, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Dkt.Janeth Makoye na Mhandisi wa halmashauri hiyo, Erick Rugeiyamu ili kupisha tuhuma zinazowakabili.
Ni juu ya matumizi mabaya ya fedha za miradi ya afya wilayani humo. Mheshimiwa Mgumba pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kufuatia matumizi mabaya ya fedha za umma katika miradi ya afya.

RC Mgumba amechukua hatua hiyo leo Septemba 14,2021 baada ya kukagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Igoye wilayani humo ambapo licha ya Serikali kupeleka shilingi milioni 50, ujenzi wa zahanati hiyo haujakamilika.

Mheshimiwa Mgumba amesema, leo alipofika alitarajia kukuta wataalamu wa afya wapo kazini wakihudumia wananchi,lakini baada ya ukaguzi akabaini kuna kasoro kubwa.

"Baada ya kukagua jengo humu ndani, sitaki kuwa mnafiki sijafurahishwa sijafurahishwa kwa kuwa mradi haujakamilika kwa wakati na nilipowauliza wataalamu wetu wameniambia sababu ni mvua, barabara mbaya, lakini tangu nifike hapa Songwe mwezi wa tano hakuna siku hata moja mvua imenyesha,”amesema Mheshimiwa Mgumba.

Pia Mheshimiwa Mgumba amesema kuwa,mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Igoye ni miongoni mwa miradi ya afya katika halmashauri hiyo ambayo imekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Amesema katika hali isiyokuwa ya kawaida licha ya Serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 50 na wananchi kujitolea nguvu kazi yenye thamani ya shilingi milioni 19 bado ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji umeshindwa kukamilika.

Mheshimiwa Mgumba amesema kuwa,haiwezekani wananchi wajenge hadi kuezeka kwa kutumia shilingi milioni 19, halafu Serikali ikaunga mkono kwa shilingi milioni 50 na wao wameshindwa kukamilisha ujenzi.

"Nasema hapa kuna matumizi mabaya, hivyo naagiza ndani ya siku saba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mnipatie taarifa. Pia kwa mamlaka niliyopewa, ofisi yangu pia itaunda kamati maalum ya uchunguzi ili ikifikia wakati wa kuchukua uamuzi tusimuonee wala kumpendelea mtu,”amesema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Zahanati hiyo ya kijiji, Ephes Kibona amemlalamikia kutishiwa maisha na baadhi ya watendaji wa halmashauri kutokana na msimamo wake wa kutaka taratibu zifuatwe kwenye ujenzi ili ikamilike haraka iweze kutoa huduma kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news