MAONESHO YA MADINI YAIBUA WABUNGE

Na Robert Kalokola,Geita

Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Nishati na Madini wamesema maonesho ya teknolojia ya uwekezaji katika sekta ya madini yatanufaisha wachimbaji wakubwa na wadogo kwa kupata elimu ya teknolojia mpya ya uchimbaji.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Nishati na Madini, Seif Gulamali baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo mjini Geita akiwa na wajumbe wa kamati hiyo.
Ameeleza kuwa, shughuli za uchimbaji wa madini zinahusisha teknolojia za aina mbalimbali, hivyo maonesho hayo yatasaidia watu wengi hasa wachimbaji kutoka Kanda ya Ziwa kujifunza teknolojia mpya ya uchimbaji.

Aidha, amefafanua kuwa shughuli za uchimbaji hasa matumizi ya Zebaki yanachangia kwa kiwango kikubwa kusababisha ugonjwa wa Saratani .

Amesema kuwa, taarifa nyingi walizo nazo ni kuwa wagonjwa wengi wa saratani wanapatikana katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, hivyo kusafiri kwenda kutibiwa jijini Dar es salaam katika Hospitali ya Ocean Road ni mzigo mkubwa kwa wagonjwa.

Ameshauri, Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kama mgodi wa kuchimba dhahabu wa Geita (GGML) kujenga Hospitali ya kutibu Saratani katika Kanda ya Ziwa ili kupambana na ugonjwa huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini akiwa kwenye maonesho ya uwekezaji katika sekta ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Mwenyekiti Seif Gulamali amesema, taasisi za Wizara ya Madini kama Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Taasisi ya Utafiti na Jiolojia Tanzania ( GST) na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi katika Sekta ya Uziduaji ( Teiti) zinaendelea kutoa huduma katika maonesho hayo kwa wachimbaji wa madini.

Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya amesema, lengo kuu la kuanzishwa kwa maonesho hayo ni kukutanisha pamoja wachimbaji wakubwa na wadogo na wadau mbalimbali katika Sekta ya Madini ili kubadilishana teknolojia.
Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya katika maonesho ya uwekezaji katika teknolojia ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Ameongeza kuwa, katika sekta ya uchimbaji kuna mambo mengi ya kujifunza ambayo yanabadilika kila siku.

Ameeleza kuwa, Wizara ya Madini ina banda katika maonesho hayo ambalo pamoja na mambo mengine ni kutoa huduma ya kutatua matatizo yote ya leseni za madini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akizungumza katika maonesho ya uwekezaji katika sekta ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema kuwa, watu watakaotembelea mabanda ya maonesho hayo watanufaika na kupata elimu kuhusu sekta ya madini.

Manufaa mengine ni pamoja na kukutana na wadau wengine katika sekta hiyo,kupata fursa za biashara na kujifunza teknolojia mbalimbali za kuchimba madini.

Amesema kuwa, wachimbaji wadogo bado wanatumia zebaki hivyo maonesho hayo yatatumika kuwapa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia mpya isiyotumia Zebaki.

Mkuu wa mkoa Senyamule ameongeza kuwa, katika maonesho hayo tahadhari zote za kujikinga na Uviko-19 zimezingatiwa.

Amesema kuwa, tahadhari kama kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono,na kuvaa Barakoa huduma hizo zimezingatiwa .

Meneja wa Mashirikiano kutoka Mgodi wa kuchimba madini ya dhahabu wa Geita (GGML), Manace Ndoroma amesema kuwa, mgodi huo unatumia maonesho hayo kuonyesha teknolojia mpya ya uchimbaji.

Katika maonesho hayo GGML ni mdhamini mkuu na mdau mkubwa wa madini nchini ambapo taarifa za Teiti zinaonesha ni kampuni inayoongoza kwa kulipa kodi kubwa katika sekta ya uziduaji nchini.
Meneja wa Mashirikiano wa GGML akizungumza katika maonesho ya uwekezaji katika teknolojia ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).

Meneja Ndoroma ameeleza kuwa, katika maonesho hayo GGML itatoa mafunzo namna wanavyotoa huduma za afya hasa wafanyakazi wanapopata ajali katika shughuli za uchimbaji.
Mtambo ( rada) unaotumiwa na GGML kwa ajili ya kupima na kufuatilia uimara wa miamba na kuta za mashimo ya machimbo mgodini ili kujua uimara wake ili kutoa taarifa kwa ajili ya kudhibiti vifusi kufunika wachimbaji. ( Picha na Robert Kalokola).

Ameongeza kuwa, pamoja na kuwa kinara wa uchimbaji nchini, pia mgodi huo unatoa huduma mbalimbali katika mkoa wa Geita na Tanzania nzima kwa mfano kufadhili matibabu ya midomo sungura, kukarabati Hospitali ya Wilaya ya Geita na mradi wa Ukimwi maarufu Kama Kilimanjaro Challenges.

Post a Comment

0 Comments