Makamu wa Rais: William Tate Ole Nasha alikuwa mchapakazi, mzalendo

NA MWANDISHI MAALUM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango ameshiriki ibada na baadaye shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji marehemu William Tate Olenasha iliyofanyika katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Septemba 30, 2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na waombolezaji mara baada ya kukamilika kwa ibada ya kumuaga aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji William Ole Nasha katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Septemba 30, 2021.

Shughuli ya kuaga mwili wa Marehemu William Ole Nasha imeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge, Dini, viongozi wa Ulinzi na Usalama pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais ametoa pole kwa wote walioguswa na msiba wa Ole Nasha na kuwaomba kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika wakati huu mgumu.

Amesema, marehemu Ole Nasha alitumia taaluma yake vizuri kuleta maendeleo kwa taifa na kuwatumikia wananchi wake wa Ngorongoro kwa moyo wake wote. 
 
Makamu wa Rais amemtaja marehemu Ole Nasha kama kiongozi alikuwa mchapakazi na mzalendo kwa nchi yake.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango akiwafariji wana familia ya marehemu, William Ole Nasha aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Ole Nasha iliofanyika katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Septemba 30,2021.
 
Aidha, Makamu wa Rais amesema, marehemu Ole Nasha atakumbukwa kwa msaada wake aliokuwa akiutoa kama Naibu Waziri katika masuala mbalimbali bungeni ikiwemo mchango wake katika kutetea muswada wa sheria ya fedha.

Awali, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amemtaja marehemu William Ole Nasha kama kiongozi aliyeamua kusoma sheria ili kuondoa changamoto zinazokabili jamii inayomzunguka ya wana Ngorongoro. 
 
Amesema Bunge limempoteza mbunge ambaye alikuwa makini na mwaminifu katika kuwatumikia wananchi wake.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango na mkewe mama Mbonimpaye Mpango wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji , William Ole Nasha shughuli iliofanyika katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Septemba 30,2021. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wakishiriki Ibada ya kumuaga aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji marehemu William Ole Nasha katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Septemba 30, 2021.
Mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji marehemu William Ole Nasha ukiwasili katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma kwaajili ya Ibada na shughuli ya kuaga mwili huo leo Septemba 30,2021.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema marehemu Ole Nasha atakumbukwa kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa weledi hapa nchini na kuaminiwa kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. 
 
Amesema Ole Nasha kwa kutumia taaluma yake ya sheria amefanya kazi ya kutuliza migogoro mingi ya uwekezaji iliokuwepo hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments