Waziri Biteko:Kokoto za Bahi zitajenga barabara ya Mzunguko Dodoma

Na Tito Mselem-WM

Imeelezwa kuwa, chanzo kikubwa cha kokoto zitakazotumika kujenga barabara ya mzunguko itakayozunguka Jiji la Dodoma na majengo mengine makubwa yanayojengwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ikiwemo mji wa Serikali-Mtumba zinatoka katika vijiji vya Mndem na Kilungule wilayani Bahi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mgogoro uliodumu kwa muda mrefu katika Kijiji cha Mndem wilayani Bahi jijini Dodoma.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 16, 2021 na Waziri wa Madini, Doto Biteko alipofanya ziara katika eneo lenye mgogoro wa muda mrefu ambalo linatumika kuzalisha kokoto zitakazotumika kwenye mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma.

“Tumekuja hapa kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya mmiliki wa leseni na mkandarasi mwenye mitambo hii ya kusaga kokoto, sitaki tena kusikia mtambo huu umezimwa eti kwa sababu ya mgogoro, sisi siyo Wizara ya Migogoro, sisi ni Wizara ya Madini,”amesema Waziri Biteko.
Moja ya mtambo unaotumika kusaga kokoto uliopo kijiji cha Mndem wilayani Bahi jijini Dodoma.
Aidha, Waziri Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya kujenga mradi wa barabara ya mzungunguko pamoja na majengo makubwa jijini Dodoma ili kukuza uchumi na kuepuka foleni jijini humo.

“Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan anataka mradi wa barabara ya mzunguko uishe kwa wakati na kwa gharama ndogo, tunavyochelewa, tunawachelewesha wananchi kupata huduma ya barabara bila sababu ya msingi,” amesisitiza Waziri Biteko.

“Tumekuja hapa kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya aliyepewa leseni na mkandarasi anayejenga mtambo huu wa kusaga kokoto, tumekubaliana na pande zote mbili kwamba mradi uanze leo na huu mtambo uliozimwa sitaondoka hapa mpaka mtambo uwashwe na uanze uzalishaji leo,” ameongeza Waziri Biteko.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto) akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (katikati) katika kijiji cha Mndem wilayani Bahi jijini Dodoma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amempongeza Waziri Biteko kwa kufika katika kijiji cha Mndem kutatua changamoto zilizokuwepo kwa kipindi kirefu ambapo amesema, amefurahi kwa kuambiwa nani aliyepewa leseni katika eneo hilo na sasa anamfahamu.

Pia, Munkunda amesema kuwa, sehemu kubwa ya madini ya ujenzi yatakayotumika katika ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko ya kilomita 110 jijini Dodoma mengi yatatoka wilaya ya Bahi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akipewa maelezo na kiongozi wa kampuni ya kusaga kokoto ya China Engineering Construction Corporation Project Dodoma Outer Ring road katika kijiji cha Mndem wilayani Bahi jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia) akizungumza jambo na Kamishna wa Madini, Dkt. Abdul-Rahman Mwanga katika kijiji cha Mndem wilayani Bahi jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto) akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya wa Bahi, Mwanahamisi Munkunda pamoja na viongozi wengine wa serikali na wilaya ya Bahi katika kijiji cha Mndem wilayani Bahi jijini Dodoma.

Munkunda amemuhakikishia Waziri Biteko kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watu wote wanaomiliki leseni katika wilaya ya Bahi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu.

Sambamba na hilo, Mwanahamisi ametoa wito kwa wawekezaji wengine kuja wilayani Bahi kuwekeza kufuatia maeneo mengi wilayani humo yanahifadhi kubwa ya madini ya ujenzi.

Post a Comment

0 Comments