USHIRIKIANO NI CHACHU YA MAENDELEO KWA WANAFUNZI – MAMA ZAINAB

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, amewakumbusha wazazi na jamii kwa ujumla, kuhakikisha kwamba wanatoa ushirikiano ipasavyo kwa walimu katika kuwasaidia watoto kupata elimu bora.
Mama Zainab ameyasema hayo huko Mfenesini Wilaya Magharib ‘A’ Unguja alipozungumza katika sherehe maalumu ya skuli ya ‘Swafaa Islamic Academy’ ya Mfenesini.

Amesema ni wajibu na jukumu la kila mzazi kushirikiana vyema na walimu ili kuhakikisha wanawasaidia watoto kupata elimu yenye manufaa na kuwajengea misingi mizuri ya maisha yao.

Amewakumbusha wazazi kufahamu umuhimu wa kuwafundisha vyema watoto elimu ya dini na dunia katika kuwajenga watoto kuwa wema, wanaoweza kuepukana na changamoto ya utandawazi inayoleta athari kubwa katika malezi na kuharibu mustakabali wa maisha yao ya baadae.

“Suala la kutoa elimu sio tu la waalimu katika vituo vya kufundishia, bali na wazazi wanamchango mkubwa kwani muda mwingi wanakuwa na Watoto hao nyumbani, hivyo ni rahisi kuyasahau hata waliyofundishwa kama hakutakuwa na uangalizi mzuri”, alifafanua.

Mama Zainab ameitaka jamii kupunguza uhuru wa matumizi ya simu kwa watoto, kwakuwa matumizi ya simu katika umri mdogo yamekuwa ni chachu kubwa ya kuleta changamoto kwa jamii katika maelezi na kuharibika maadili.

Mke huyo wa Makamu wa Kwanza, aliahidi kusaidiana na uongozi wa skuli hiyo katika kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili hasa kwa kuzingatia kwamba kila mmoja ndani ya jamii anawajibu wa kuchangia maendeleo ya elimu kwa watoto.

Mama Zainab ametoa wito kwa jamii kujikita katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto ili kuwawekea mazingira salama.

Aidha Mama Zainab ambaye pia ni mlezi wa vituo mbali mbali vya Watoto yatima na wenye mahitaji maalum, ameahidi kusaidia huduma kwa watoto wenye changamoto hio.

Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Bi. Salma Ali Khamis, aliitaka jamii kuzingatia umuhimu wa kujenga mashirikiano imara baina ya walimu na wazazi kwa kuwa yanaongeza uwezo na juhudi za Pamoja katika kuwapatia watoto elimu yenye manuafaa kwa sasa na baadae.

Amesema kwamba jitihada za pamoja ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa vyema watoto kielimu, sambamba na kuwaweka wazi watoto kwa kuwaeleza na kuyafahamu mambo yanayosababisha changamoto za kuvuruga utaratibu wao wa kupata elimu bora.

Katika risala yao iliyosomwa na mwalimu wa skuli hiyo, Bi. Asha Jaku walisema kwamba Skuli yao imekabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo maji na vifaa vya kisasa vya kufundishia.

Walimuomba mgeni rasmi kusaidia kupatikana ufumbuzi kwa changamoto mbali mbali za skuli hiyo ili kuhakikisha kwamba wanatimiza malengo ya kuwafundisha na kuwalea vyema watoto.

Aidha walimuomba Mke huyo wa Makamu wa kwanza wa Rais, Kukubali kuwa mlezi wa skuli hiyo ombi ambalo limekubaliwa

Mapema katika katika hafla hiyo wanafunzi walifanya maonesho ya vipaji vya kusoma Quran, hadithi na mambo mbali mbali ya kuendeleza dini ya kiislamu na dunia, ambapo washiriki walikabidhiwa zawadi mbali mbali ikiwemo fedha na vifaa vya kusomea.

Post a Comment

0 Comments