Wanachama wa Chama cha Waepidemiolojia Tanzania wafanya usafi hospitalini

Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog

Kufuatia Chama cha Waepidemiolojia Tanzania (TANFLEA) kuadhimisha Siku yao Duniani, jijini Dodoma wameamua kufanya usafi katika Hospitali ya Rufaa Mkoa ikiwa ni sehemu ya kuhamasaisha jamii kufanya usafi hasa kipindi hiki Dunia inapokabiliwa na janga la UVIKO-19.

Mwakilishi wa chama hicho, Mwanaepidemiolojia,Boniphace Mhabe akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa mara baada ya zoezi hilo la usafi amesema kuwa, chama hicho kimejizatiti kuhakikisha kinatoa huduma mbalimbali kwa jamii.

Amesema, katika kuadhimisha maadhimisho hayo waliweza kutoa elimu ya afya,uchangiaji damu, kupima afya na hatimaye kufanya usafi katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji.

"Sisi kama watafiti na makachero wa magonjwa wakati tunapofanya uchunguzi wa milipuko mbalimbali ya magonjwa moja kati ya visababishi ambavyo tumeviona vikisababisha magonjwa mbalimbali ni kutozingatia usafi hasa milipuko ya kipindupindu.

"Na hata sasa tunapopambana na UVIKO-19 tumeona ni vyema tuzingatie masuala ya usafi, hivyo sisi kama Chama Cha wa Waepidemiolojia Tanzania tumeona ni muhimu sana kama sehemu ya kuhamasisha jamii hasa eneo la hospitali ambapo wananchi wanakuja kwa wingi na ukizingatia kwamba mtu anaweza kuja kutibiwa na malalia, lakini akaondoka na ugonjwa mwingine kwa sababu ya mazingira kuwa machafu,"amesema Mhabe.

Ametoa wito kwa jamii kuzingatia masuala ya usafi na elimu za afya,chanjo zinazotolewa na wizara husika huku akidai kwamba jamii inapaswa kutambua chama chao ambacho kinajihusisha hasa na kuchunguza, kufuatilia na kushauri namna ya kudhibiti magonjwa yote yale ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General), Daktari Stanly Mahundo amesema kuwa,zoezi hilo limekuwa chachu ya kuhamasisha usafi.

"Kwa niaba ya hospital tunawashukuru sana Chama cha Waepidemiolojia Tanzania kwa zoezi hili la usafi na vifaa hivi mlivyotupatia.

"Niwasihi vikundi vingine waige mfano huu, kwani kuna maadhimisho mengi yanafanyika, lakini huwa hawako tayari kufanya jambo hili mlilolifanya,tuwaahidi kwamba tutahakikisha tunashirikiana na nyie katika huduma hizo za afya,"amesema Mahundo.Hata hivyo vifaa hivyo ni pamoja na majembe,mabuti,mafagio,reki na mafekeo.

Post a Comment

0 Comments