Waziri Ummy atoa maelekezo kuhusu wanafunzi wote watakaofaulu

Na Rotary Haule, Kibaha

WAZIRI wa Nchi ,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu ameitaka Halmashauri ya Kibaha Vijijini kuhakikisha wanafunzi wote watakaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 wanaanza shule kwa pamoja.
Mwalimu ametoa kauli hiyo katika ziara yake aliyoifanya katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini ikiwa na lengo la kujua namna wanavyosimamia mapato ya ndani na hata kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Shule mpya ya Sekondari Disunyara.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga vizuri katika suala la elimu na kwa kuanzia wamepanga kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu wanaanza shule mara moja.

Amesema kuwa,hakuna sababu ya kushindwa kuwapokea wanafunzi waliofaulu kwa kigezo cha kukosa madarasa au madawati jambo ambalo ni uzembe kwakuwa muda wa kujiandaa upo.

Ameongeza kuwa,mara nyingi kumekuwa na tabia ya wanafunzi wengine kusubiri chaguo la pili (Second Selection) na kusema kwa mwakani jambo hilo halitakuwepo wanafunzi wote waliofaulu watachaguliwa maramoja.

Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini, Butamo Ndalahwa kuanza mapema mchakato wa kujenga madarasa pamoja na kukabiliana na changamoto nyingine za kielimu ili kusudi ifikapo mwakani wanafunzi wote wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza wawe darasani.

Amesema kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kupeleka kila jimbo shilingi milioni 600 ambazo zitatumika kujenga Shule moja ya Sekondari na kwa upande wa Kibaha Vijijini shule hiyo itajengwa Kata ya Gwata.

"Serikali ya Awamu ya Sita imepanga kutoa shilingi milioni 600 kila jimbo kwa ajili ya kujenga sekondari moja, lakini kwa hapa Kibaha Vijijini shule hiyo itajengwa Kata ya Gwata kwa hiyo naomba halmashauri ijipange vizuri kusimamia ujenzi huom,"amesema Ummy.

Aidha,Ummy ameongeza kuwa, kwa hatua ya awali ya ujenzi wa shule hiyo Kibaha Vijijini itapewa sh.milioni 465 na baadae kumalizia kiasi kilichobaki na kusema shule hiyo itakuwa madarasa manne na maabara moja.

Mbali na kutembelea shule hiyo, lakini pia Waziri Ummy alitembelea eneo la Kisabi linalokusudiwa kujenga mradi wa soko na stendi ya mabasi katika Mji wa Mlandizi ambapo hata hivyo hakuweza kulitolea maamuzi na badala yake alishauri kupata majibu ya kutoka ofisi ya mazingira (NEMC).

"Nimetembelea eneo la ujenzi wa soko na stendi hapa Kisabi Mlandizi, lakini naomba nisitolee maamuzi leo, lakini nashauri tusubiri tamko kutoka wataalamu wa ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira (NEMC) ili tukijenga tusiwe na shaka," amesema Waziri Ummy.

Aidha,Waziri Ummy amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, kushughulikia jambo hilo na baadae apewe mrejesho ndani ya wiki mbili ili kusudi mchakato na maamuzi ya kujenga soko hilo uanze maramoja.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini, Butamo Ndalahwa amesema kuwa, amepokea maagizo hayo na ameahidi kusimamia utekelezaji huo kwa kuhakikisha watoto wote watakaofaulu wataanza kidato cha kwanza kwa wakati mmoja.

"Mheshimiwa Waziri wa Tamisemi Halmashauri yetu imejipanga vizuri na tutahakikisha wanafunzi watakaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wote watawapeleka shule bila tatizo,"amesema Ndalahwa.

Awali akizungumza katika kikao cha Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani kilichowajumuisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maofisa wengine Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alimueleza Waziri huyo kuwa Pwani imejipanga kikamilifu kutatua changamoto katika jamii.

Kunenge amesema, Mkoa wa Pwani una changamoto nyingi ikiwemo migogoro ya ardhi, lakini ina fursa kubwa ya uwekezaji katika viwanda na kwamba wapo tayari kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuweza kusaidia jamii na hata kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kuijenga nchi.

Post a Comment

0 Comments