WAZIRI MKUU AKATAA KUFUNGUA OFISI YA TANESCO KYERWA

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo yaliyopo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza taarifa ya ujenzi wa ofisi ya TANESCO wilaya ya Kyerwa iliyokuwa ikisomwa na Meneja Mwandamizi Usambazaji wa TANESCO, Mhandisi Natthanasias Nangali (wa tatu kushoto), hata hivyo Mhe. Majaliwa alikataa kufungua ofisi hiyo kama alivyopangiwa katika ratiba ya ziara yeke mkoani Kagera. Septemba 20, 2021, baada ya kubaini kuwa gharama za ujenzi wake ni kubwa. Kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, wa tano kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato na wa sita kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).

“Nikiweka jiwe la msingi nitakuwa nimehalalisha majengo mengine yajengwe kwa gharama hii. Siwezi kuweka jiwe la msingi, gharama zilizotumika ni kubwa kuliko majengo yaliyopo. Simamieni ujenzi wa majengo yenu na mjenge kwa kutumia mfumo wa force account.”

Mheshimiwa Majaliwa amekataa kufungua ofisi hiyo leo Septemba 20, 2021 wakati akiwa katika katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

“Nini kilisababisha hadi kibanda kigodo cha mlinzi kikajengwa kwa shilingi milioni saba? Kina matofali mangapi kama sio ulaji nini? hii si sahihi sijaweka jiwe la msingi wala kufungua na kile kibao kilichoandikwa jina langu kiondolewe. Serikali ipo makini katika usimamizi wa miradi na haya ni maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.”
Muonekano wa jengo la ofisi ya TANESCO wilaya ya Kyerwa ambalo limejengwa kw gharama ya shilingi milioni 253.8 ambalo Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa alikataa kufungua kama alivyopngiwa kwenye ratiba ya ziara yeke mkoni Kagera, Septemba 20, 2021 baada ya kubaini kuwa limejengwa kwa gharama kubwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akiwa amezungukwa na viongozi pamoja na Waandishi wa Habari wakati alipokagua kibanda cha mlinzi katika lango kuu la kuingia eneo la Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Kyerwa ambacho kimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 7.03. 

Mheshimiwa Majaliwa alikataa kufungua ofisi hiyo kama livyopngiwa kwenye ratiba ya ziara yeke mkoni Kagera, Septemba 20, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mradi wa ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 483.42, ambapo kibanda cha mlinzi kimegharimu shilingi milioni 7.03, uzio shilingi milioni 94.2, jengo la ofisi shilingi milioni 253.8 na stoo shilingi milioni 51.55.

Waziri Mkuu amesema Serikali inajenga majengo makubwa ya vituo vya afya ambayo ni jengo la mapokezi ya wagonjwa, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, nyumba ya daktari, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka na korido kwa gharama ya shilingi milioni 500.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa TANESCO uhakikishe katika miradi yake mingine ya ujenzi gharama zilingane na aina na idadi ya majengo.
Kibanda cha Mlinzi kilichopo kwenye lango kuu la kuingia katika ofisi ya TNESCVO ya wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera ambacho kimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 7.03. Mheshimiwa Majaliwa alikataa kufungua Ofisi hiyo kama livyopngiwa kwenye ratiba ya şziara yeke mkoni Kagera, Septemba 20, 2021 baada ya kubaini kuwa limejengwa kwa gharama kubwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO, Ofisi ya Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera kabla hajakataa kuifungua ofisi hiyo kama alivyopangiwa kwenye ratiba ya ziara yake Mkoani Kagera baada ya kubaini kuwa gharama zilizotumika kujenga ofisi hiyo ni kubwa. Wa pili kulia ni Mkewe Mary Majaliwa na kulia ni Meneja Mwandamizi Usambazaji wa TANESCO, Mhandisi Natthanasias Nangali . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Jengo la Stoo ya ofisi ya TANESCO wilaya ya Kyerwa ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni. 51.55. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikataa kufungua ofisi hiyo kama livyopngiwa kwenye ratiba ya ziara yeke mkoani Kagera, Septemba 20, 2021 baada ya kubaini kuwa imejengwa kwa gharama kubwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Naye, Meneja Mwandamizi Usambazi wa TANESCO Makao Makuu, Mhandisi Nathanasias Nangali ambaye alisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, amesema mradi huo ulianza Septemba 11, 2018 na kukamilika Februari 08, 2020 kwa gharama za shilingi 483,422,328.02.

Amesema mkandarasi aliyenga mradi huo ni kampuni ya M/S RK Ivestment chini ya usimamizi wa mkandarasi mshauri TANESCO kitengo cha miliki. “TANESCO imeendelea kutumia wataalamu wake katika kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa ofisi zake za mikoa, wilaya na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.”

Amesema TANESCO imeendelea kutenga fedha kwa awamu kila mwaka ili kutekeleza miradi kama hiyo ambapo katika mwaka huu inaendelea na ujenzi wa ofisi za wilaya za Buhigwe-Kigoma, Ruangwa-Lindi, Urambo-Tabora, Gairo na Malinyi-Morogoro, Nanyumbu na Tandahimba-Mtwara, Kilolo-Iringa, Rorya na Serengeti-Mara, Laela-Rukwa na Meatu-Simiyu.

Akizungumzia huduma ya umeme inayotolewa katika wilaya hiyo amesema kati ya vijiji 99 vya wilaya hiyo vijiji 70 vinaumeme na vijiji 29 vilivyosalia vitapata huduma hiyo kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unaoendelea kutekelezwa.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea na kukagua kiwanda cha kuchenjua madini ya bati (TIN) cha kampuni ya African Top Minerals kilichopo wilayani Kyerwa ambapo alitumia fursa hiyo kumuhakikishia mwekezaji huyo kwamba Serikali itaendelea kumuunga mkono.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hassan Ibar alisema mradi huo uliogharimu shilingi bilioni nne unalengo la kuboresha na kukuza sekta ya madini wilayani Kyerwa na Tanzania kwa kuongeza thamani ya madini hayo katika soko la dunia, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi.

Aliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kutambua mchango wa madini ya bati kwa kuzindua cheti cha uhalisia cha madini hayo ambacho kimewasaidia kutambulika kimataifa na kufanya biashara yao kwa uhakika.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia kwa jitihada zake za kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji, tutaendelea kumuunga mkono.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news