Familia ya kijana Mtanzania Humphrey Magwira aliyeuawa kwa kupigwa risasi Marekani yafunguka mengi

HOUSTON,Familia ya Kijana Mtanzania Humphrey Magwira aliyeuawa kwa kupigwa risasi siku ya Ijumaa kufuatia ajali ya gari alilokuwa akiendesha kugonga gari ndogo katika eneo la Fort Bend, Houston imesema kijana wao atazikwa nyumbani nchini Tanzania na kuomba ndugu jamaa na marafiki kusaidia kuwezesha kusafirisha mwili wa marehemu.
Humphrey (20) alifariki muda mchache kabla ya kufikishwa hospitalini. Alishambuliwa na kijana aliyefahamika kwa jina la Ramon Vasquez (19) ambaye alikamatwa Jumamosi ya Oktoba 16 na kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Humphrey alikuwa akisomea uhandisi wa kompyuta katika chuo kikuu cha Houston.

MKASA NI HUU

Ijumaa ya Oktoba 15, Humphrey ambaye ni Mwanafunzi wa Uhandisi wa Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Houston, Marekani alifikwa na mauti baada ya kushambuliwa na risasi mfululizo katika makutano ya Barabara ya Beechnut na Addicks Clodine yaliyopo Kaunti ya Fort Bend.

Polisi wamedai tukio hilo limetokea eneo karibu na alipokuwa anaishi, yeye na wazazi wake. Inadaiwa wakati marehemu alipogonga gari la Ramon, kijana huyo alishuka katika gari alilokuwa akiendesha na kuanza kummiminia risasi. Muda mchache baadae alitoweka katika eneo la tukio kwa kutumia gari lake akimuacha Humphrey mahututi.

Polisi wa Kauti ya Fort Bend walijaribu kumkimbiza hospitali ili waokoe maisha yake lakini, walivyofika hospitalini, madaktari walimtangaza kuwa alishafariki dunia.

Uchunguzi wa tukio uliendelea, na maafisa wa polisi walifanikiwa kumnasa mshukiwa asubuhi ya Jumamosi, Oktoba 16 na kumfungulia kesi ya mauaji.

Ramon bado yuko kizuizini ingawa polisi wametangaza dhamana ya kiasi cha Dola za Marekani 500,000 sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.152. Wazazi wa marehemu wametaka haki dhidi ya Humphrey itendeke.

Kaka wa marehemu, Rodricque ameanzisha kampeni kuhamasisha watu kuchangia gharama za kusafirisha mwili wa marehemu kupitia mtandao ‘GoFundMe’ na akaunti ya simu (0715447436- na 0754447436) zote zimesajiriwa kwa jina la Janet Kuyangana.

Kwa siku tatu toka Rodricque afungue kampeni hiyo wachangiaji 464 walikuwa wamechangia $226758 sawa na zaidi ya Sh milioni 52.45.

“Mtu huyo alimpiga risasi kaka yangu mara sita bila Majuto... Ndugu yangu hakufa tu bali aliuawa bila sababu ya msingi kutolewa,” ameandika Rodricque.
Mama wa Marehemu amesema Humphrey alikuwa rafiki yake mwenye ndoto kubwa. “Tulikuja Marekani ili kuwapa maisha bora watoto wetu lakini ameuawa kinyama,” alisema baba wa marehemu katika mahojiano na waandishi wa Habari.

Humphrey alihamia Marekani miaka Nane iliyopita. Mbali na kupenda kompyuta alikuwa akipenda mpira. (Habari Leo).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news