Maagizo ya Rais Dkt.Mwinyi kwa Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi na kusisitiza haja ya kwenda kuzitangaza fusra za kujenga uchumi wa nchi ikiwemo Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio dira ya uchumi wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Mabalozi waliopishwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tannzania katika Nchi mbali mbali walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo (pichani wa pili kulia) Mhe.Balozi Anisa Mbega Nchini India (katikati) MheInnocent Shiyo Nchini Afrika ya Kusini na (kushoto) Mhe.Togolani Mavura Nchini Korea Kusini.

Mabalozi ambao amekutana nao Rais Dkt.Mwinyi Ikulu jijini Zanzibar leo Oktoba 25,2021 na kufanya nao mazungumzo ni Balozi Anisa Mbega anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini India, Balozi Togolani Edriss Mavura anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Korea Kusini na Balozi Innocent Shiyo anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt.Mwinyi amewaeleza mabalozi hao kwamba nchi kama Korea Kusini imepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika kuitumia bahari kama sehemu moja wapo ya kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuwa na viwanda vingi vya uvuvi, bandari na viwanda vya meli hatua ambayo inaweza kusaidia katika kuendeleza Sera ya Uchumi wa Buluu kwa Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza haja kwa mabalozi hao kwenda kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na vivutio vyake kadhaa vilivyopo hasa kwa nchi za Korea Kusini na India ambako bado watalii wake wanaokuja kuitembelea Zanzibar hawajawa wengi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Mabalozi waliopishwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Tannzania Nchi mbali mbali walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha.

Rais Dkt.Mwinyi amewaeleza Mabalozi hao juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wake kupitia ujenzi wa bandari ya kisasa ambayo itajumuisha shughuli mbali mbali ambapo pia, itahitaji wawekezaji.

Ameeleza mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha inaijengea uwezo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) iweze kufanya kazi ipasavyo na kuwa kituo maalum kitakachotoa huduma zote za uwekezaji kwa muda mfupi sambamba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi waliopishwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tannzania Nchi katika mbali mbali walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo,(kushoto) Mhe.Balozi Togolani Mavura Nchini Korea Kusini,Mhe.Anisa Mbega Nchini India na Mhe.Innocent Shiyo Nchini Afrika ya Kusini pia na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Injinia Zena Ahmed Said (kulia). (Picha zote na Ikulu).

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza haja kwa Mabalozi hao kusaidia kutafuta soko kwa ajili ya zao la mwani kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo sanjari na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuja kuekeza katika sekta ya viwanda pamoja na gesi asilia hapa Zanzibar.

Nao mabalozi hao kwa upande wao wamemuhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kuwa juhudi za makusudi watazichukua katika kuhakikisha wanatekeleza vyema majukumu waliyopewa na kutumia fursa hiyo kutoa shukurani zao kwa Rais kutokana na maelekezo aliyowapa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news