TARURA Pwani watiliana saini ya mikataba na wakandarasi 17

NA ROTARY HAULE

WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Pwani wametiliana saini ya mikataba 17 yenye thamani ya sh.bilioni 6.2 na wakandarasi mbalimbali waliopo mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Mkurugenzi wa Isimila Company Limited, Mhandisi Anjela Shayo (kulia) akibadilishana hati ya mkataba wa utekelezaji wa ujenzi wa barabara na Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji katika hafla ya kutiliana saini ya mikataba na wakandarasi 17 wa Mkoa wa Pwani.Hafla hiyo imefanyika mjini Kibaha leo na anayeshuhudia mbele ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge. (NA ROTARY HAULE).

Hafla hiyo imefanyika leo Mjini Kibaha huku ikishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge,Katibu Tawala wa Mkoa, Mwanasha Tumbo,wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri,wenyeviti pamoja na sekretarieti ya Mkoa wa Pwani.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji amesema kuwa mikataba 17 iliyosainiwa leo inakwenda kuongeza idadi ya mikataba na kufikia mikataba 74 itakayotekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22.

Mhandisi Runji amesema kuwa, mikataba hiyo itatekelezwa kwa fedha ambazo zitatoka maeneo mawili tofauti ikiwemo fedha za kawaida na fedha za mfuko mkuu wa Serikali huku akisema mpaka sasa TARURA Pwani imepokea sh.bilioni 2.2 kwa ajili ya utekelezaji huo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza mara baada ya kushuhudia zoezi hilo amesema kuwa, kuwepo kwa miundombinu mizuri kutafungua fursa ya uchumi kwa wananchi.
Kunenge amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya barabara huku akitaka wakandarasi kufanyakazi kwa uadilifu.

Amesema kuwa, wakandarasi wanaopewa tenda wahakikishe wanamaliza kazi kwa wakati na ikiwezekana kazi wanazofanya ziwe za viwango kulingana na fedha walizopewa.

"Nataka wakandarasi wafanyekazi masaa 24 na mimi nitakuwa napita huko kukagua hata usiku lakini kikubwa ninachotaka kuona kazi zote zinatekelezwa kwa kiwango kuendana na thamani ya fedha,"amesema.

Aidha, Kunenge ameongeza kuwa, Serikali inawapenda wakandarasi wazalendo, lakini wakati mwingine wamekuwa kero kwa kuwa wanashindwa kukamilisha miradi huku akisema wakandarasi wazembe lazima watachukuliwa hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine Kunenge amewataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi na viongozi wengine kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo kikamilifu na kamwe wasimvumilie mtu anayehujumu miundombinu ya barabara inayojengwa.

"Wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri hakikisheni miradi inakamilika kwa wakati, lakini msiwe kero kwa wakandarasi,waacheni wafanye kazi kwa uhuru na asitokee mtu anakwenda kuomba fedha kwa wakandarasi au kumtisha kwa madai bila yeye asingepata tenda,"amesema Kunenge.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno amewataka wakandarasi kujenga uaminifu kwa Serikali kwa kuhakikisha wanajenga miradi yenye ubora.

Maneno amesema wakifanya vizuri ni wazi kuwa watakuwa wamekisaidia chama kwa kuwa ndio chama kinachoisimamia Serikali huku akisisitiza mgawanyo wa fedha uwe wa usawa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news