Maagizo ya Rais Samia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAKUKURU

NA GODFREY NNKO

Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuifanyia kazi taarifa ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na kuwachukulia hatua stahiki wale wataobainika kuhusika na ubadhirifu katika miradi iliyotajwa kuwa na kasoro. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa kwenye kilele cha mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021 zilizofanyika leo Oktoba 14,2021 katika Uwanja wa Magufuli Wilayani Chato Mkoani Geita. (PICHA NA IKULU).

Mhe. Rais Samia, amesema hayo leo tarehe 14 Oktoba, 2021 wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru, Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Nyerere na Wiki ya Vijana yaliyofanyika katika viwanja vya Magufuli wilayani Chato Mkoani Geita.

Amesema haiwezekani kufikia maendeleo kama taifa litaendelea kuwa na vitendo vya rushwa na ufisadi, kwani vitendo hivyo ni chanzo cha ukiukwaji wa haki za wananchi, kuwepo kwa mikataba mibovu na ukiukwaji wa taratibu za ujenzi katika miradi ya maendeleo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema amekuwa akijiuliza kwa nini viongozi wa maeneo ambayo miradi iliyokutwa na dosari ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maofisa TAKUKURU na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wapo lakini wanasubiri mpaka wakati mbio za mwenge wa Uhuru zipite ndipo wabaini dosari za miradi hiyo.

Mhe. Rais Samia ametoa tahadhari kwa miradi inayokwenda kutekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo kwa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 kuwa lisijitokeze suala la ubadhirifu na kuwa atasimama imara kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo na miradi mingine.

Pia Mhe. Rais Samia amewataka viongozi katika maeneo utakapopita Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 kuhakikisha idadi ya miradi yenye dosari inapungua.

Akizungumzia juu ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, amesema Serikali itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, kutokana na ujasiri alioukuwa nao ukiwemo ushupavu wa kuitumikia nchi yake.

Kuhusu sekta ya afya, Mhe. Rais Samia amesema bado hali haiko vizuri kutokana na kuongezeka kwa maradhi yasio ya kuambukiza yakiwemo ya shinikizo la damu, Kisukari, Kifua Kikuu, Ukimwi, Malaria na janga la UVIKO 19, jambo ambalo ni vyema kwa vijana wa Tanzania kuendelea kuchukua tahadhari ya maradhi hayo.

Mhe. Rais Samia, amewataka wananchi kujikinga na UVIKO 19 kwa kuona umuhimu wa kuchanja kwani Serikali tayari imeshasambaza chanjo na kuwaasa vijana kuacha kutumia dawa za kulevya kutokana na athari zake kwa afya.

Mwenge huo wa Uhuru umetembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 1, 067 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.2 kutoka sekta za maji, nishati, afya, kilimo, uvuvi, mifugo na miundombinu.

Mapema alipowasili Wilayani Chato, Mhe. Rais Samia alizuru na kuweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwao Chato mkoani Geita.

Maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru zimefanyika Wilaya ya Chato Mkoani Geita ili kumuenzi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia leo ameanza ziara ya siku tatu mkoani Kilimanjaro ambapo pamoja na masuala mengine atafungua miradi mbalimbali ya maendeo na kuzungumza na wananchi mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news