Rais Mwinyi awaalika wawekezaji wa Kimataifa kuja kuwekeza nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaalika wawekezaji kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nyingine duniani kuja kuwekeza Zanzibar na Tanzania Bara.
Amesema hayo wakati akifunga Onesho la Kwanza la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoanza Oktoba 9, mwaka huu na kuhitimishwa jijini Arusha.

Aidha, amesema kuwa katika visiwa vya Zanzibar kuna maeneo mengi ya uwekezaji hususan katika uchumi wa Buluu kupitia bahari na maeneo mengine kama ya utalii wa kitamaduni.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, nchi za EAC zina vivutio vilivyopo karibu kila eneo, hivyo nchi hizo zifanye jitihada kuwavutia watalii wengi zaidi ili vivutio hivyo vichangie zaidi katika maendeleo ya nchi hizo.

Amesema, katika nchi za EAC, pia kuna vivutio vingi vilivyopo karibu kila eneo, hivyo nchi hizo zifanye jitihada kuwavutia watalii wengi zaidi ili vivutio hivyo vichangie zaidi katika maendeleo ya nchi hizo.

“Ripoti ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) inaonesha kwamba idadi ya watalii wanaokuja ni asilimia 8.6 ya watalii wote wanaokuja Bara la Afrika wakati idadi hiyo ni sawa na asilimia 0.3 ya watalii wote duniani,” amesema Dkt.Mwinyi.

Amesisitiza kwamba idadi hiyo ni ndogo kulingana na watalii wanaokuja Afrika, hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuongeza idadi ya watalii zaidi.

Amesisitiza jitahada zaidi kufanyika ili kuongeza idadi ya watalii hasa baada ya janga la Covid-19 kujitokeza na kwamba licha ya janga lazima utalii na vivutio vyake utangazwe ili kuhakikisha watalii wengi zaidi wanakuja katika nchi za EAC ikiwamo Tanzania.

Amesema, kwa sasa mapato yanayotokana na utalii hayaendani na wingi na ubora wa vivutio vya utalii vilivyopo na akasema nchi za EAC ikiwamo Tanzania zina utajiri wa vivutio vya utalii vikiwamo hasa vya asili.

Amezihimiza nchi za EAC kuboresha sera za utalii ili kusaidia wawekezaji katika sekta ya utalii kufanya kazi kwa ufanisi.

Amesema, Serikali inasisitiza uchumi wa bluu kwani zipo fursa za kuwekeza katika hoteli, meli za kitalii, michezo ya bahari na masuala mengine ya utalii na uchumi.

Amesema, Zanzibar imefungua fursa nyingi za uwekezaji ukiwemo uvuvi katika bahari kuu,majengo, utafutaji wa mafuta na gesi na kusisitiza kuwa, Zanzibar ni njema na anayetaka aje.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesisitiza kuwa,sekta ya utalii katika EAC, imeleta sura mpya kwa nchi hizo katika masuala ya utalii.

Amesema, onesho kama hilo litafanyika mwakani nchini Burundi na kuwa baada ya onesho hilo kumalizika jana, waoneshaji watapata fursa za kwenda kutembelea vivutio vya utalii vya hifadhi za taifa za Mkomazi, Serengeti, Mlima Kilimanjaro,Ngorongoro na vivutio vingine vya utalii vilivyopo Zanzibar.

Dkt.Ndumbaro amesema, onesho hilo limewashirikisha waoneshaji wakubwa wa bidhaa za utalii zaidi ya 100 huku waoneshaji 41 wakitoka katika nchi 19 za Afrika, Ulaya na Marekani. Nchi zote sita wanachama wa EAC zilishiriki na hivyo kufanya jumlaya nchi 25 zilizoshiriki.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Forodha na Biashara wa EAC, Kenneth Bagamuhunda kwa upande wake amesema kuwa, maonesho hayo yalipaswa kuanza mapema, hivyo kwa mwanzo huo mzuri unaonesha mwamko wa kuungana pamoja kwa nchi za EAC katika kutangaza utalii kwa kila nchi.

Post a Comment

0 Comments