Rais Samia aelezea mwelekeo wa Serikali yake kuhusu masuala ya sheria

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 28 Oktoba, 2021 amezindua Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu (The Tanzania Gender Bench Book on Women’s Rights) nchini Tanzania kuhusu haki za wanawake, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuzindua rasmi Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu Wanawake katika kutekeleza utoaji wa maamuzi na utendaji haki kwa familia. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 28 Oktoba, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. Kushoto Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, wa pili kushoto Mwakilishi mkazi wa UN Women hapa nchini bibi. Hodan Addou, kulia Balozi wa Sweden nchini Bw. Anders Sjoberg na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) Jaji Joaquine De Mello.

Mhe. Rais Samia amesema Kitabu hicho ambacho kimeandaliwa na wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) kwa hisani ya UN Women na Ubalozi wa Sweden, kitakuwa msaada mkubwa sio tu kwa wanawake na watoto bali kwa jamii nzima hususan katika masuala ya haki.

Mhe. Rais Samia amewapongeza TAWJA kwa kuandaa kitabu hicho kinachotoa muongozo wa namna ya kulinda haki za wanawake na watoto pamoja na kukuza utawala wa sheria hapa nchini.

Mhe. Rais Samia amesema Kitabu hicho pamoja na mambo mengine, kitatoa rejea rafiki na ya haraka kwa lengo la kuwarahisishia watoa maamuzi kulinda haki za wanawake na watoto.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiondoa kitambaa kuzindua rasmi Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu Wanawake katika kutekeleza utoaji wa maamuzi na utendaji haki kwa familia. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 28 Oktoba, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa UN Women hapa Nchini Dkt. Hodan Addou, Balozi wa Sweden Nchini Bw. Anders Sjoberg, Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) Jaji Joaquine De Mello na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante O. Gabriel.

8-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na Balozi wa Sweden Nchini Bw. Anders Sjoberg mara baada ya kuzindua rasmi Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu Wanawake katika kutekeleza utoaji wa maamuzi na utendaji haki kwa familia, Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Oktoba, 2021.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema mwongozo huu utasaidia kuongeza dhamira na nia ya dhati ya kuimarisha muitikio chanya wa masuala ya kijinsia katika maamuzi ya Mahakama na vyombo vingine vinavyoshughulika na utoaji haki.

Mhe. Rais Samia amesema Kitabu hiki kimekuja wakati muafaka ambapo Mahakama imeshakamilisha ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kwa maswala ya familia.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu wote wanaoshughulikia mashauri ya kutelekeza, mirathi, dhuluma, udhalilishwaji na unyanyaswaji kutumia kitabu hicho kama miongoni mwa miongozo itakayotumiwa na Mahakama ya masuala ya familia.

Mhe. Rais Samia amesema ana imani kuwa kitabu hicho kitasaidia kuibua haki nyingi za wanawake na watoto zinazojulikana kwa watu wengi na zile ambazo hazijulikani na walio wengi. Pia kitasaidia kuwapa watoa haki ujasiri wa kutoa maamuzi yatakayopelekea kuzika baadhi ya mila, desturi na imani potofu zinazokandamiza na kupora haki za makundi muhimu katika jamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda uliowasilishwa na Mjumbe Maalum ambae pia ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia na Ubunifu nchini Uganda Dkt. Monica Musenero Masanza, Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Oktoba, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 28 Oktoba 2021 ameshiriki katika mjadala kuhusu Kipindi cha mpito wa haki wa tabianchi ulioendeshwa kwa njia ya mtandao na Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni, Tony Blair Institute for Global Change. (PICHA NA IKULU).

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha anajenga nchi inayoheshimu na kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora kwa maendeleo ya wote kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Mhe. Rais Samia amewaomba TAWJA na wadau wote walioshiriki katika uandaaji wa Kitabu hiki kuhakikisha kuwa kitabu hicho kinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo inaeleweka kwa wengi hususan kwenye mifumo ya utoaji haki.

Pia Mhe. Rais Samia amesisitiza kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika mienendo ya mashauri na hukumu kwasababu tayari Bunge lilishafanya marekebisho ya Sheria kuruhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sheria hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news