Jumuiya ya Maridhiano yahamasisha wananchi kujitokeza kuchanja

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JUMUIYA ya Maridhiano Tanzania, Mkoa wa Mwanza imewaasa wananchi mkoani humu na Watanzania wa maeneo mengine nchini kumwunga mkono, Rais Samia Suluhu Hassan,na kujitokeza kuchanja ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona (Covid-19).
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Mkoa wa Mwanza, Sheikhe Musa Karwanyi (wa kwanza kulia),akizungumza kwenye kikao kazi cha jumuiya hiyo kuhusu uhamasishaji wananchi kuchanjwa.

Rai hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa jumuiya hiyo baada ya kikao kazi kilichofanyika kwenye Bwalo la Polisi, Mabatini jijini Mwanza na kuwashirikisha viongozi wa wilaya za Nyamagana,Sengerema,Misungwi na Ilemela.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Mwanza,Sheikhe Musa Karwanyi, alisema Watanzania na wananchi wanapaswa kumwunga mkono Rais Samia na kwenda kuchanja ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Uviko-19.

“Tumepitia changamoto nyingi za ugonjwa wa Uviko-19 na tumepoteza ndugu zetu kwa ugonjwa huo,sisi viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano tusibaki nyuma kwenye vita hii,tumwuunge mkono Mheshimiwa Rais Samia,tukawe mfano kwenye mkoa na wilaya zetu kuhamasisha watu kuchanja,”alisema.

Sheikhe Karwanyi alisema kuwa kama chanjo hiyo haikuwa salama isingewezekana Rais Samia,kujitosa kwenye hatari ya kuchanjwa na kuhatarisha maisha yake,hivyo watu wanaopinga chanjo kuwa si salama hawana nia na dhamira njema na Tanzania.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Mariadhiano mataifa tajiri wananchi wake wamepoteza maisha lakini Tanzania kwa umoja na imani tunazidi kuliombea taifa ili Mwenyezi Mungu atuondolee balaa hilo na kusisistiza nchi yetu ni masikini kwa taswira na tunachanje bure bila kulipa hata senti ilhali mataifa mengine wakichanja kwa gharam kubwa.

Kwa upande wake,Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mchungaji Robert Mloya, alisema watu wasiolitakia mema taifa letu wanajaribu kuingiza hofu kwa Watanzania lakini ukweli wao wasomi na wataalamu wa afya na kada zingine wamechanja ili kujikinga na kwamba yeye amechanja na hajapata mabadiliko wala athari za kiafya kutoka na chanjo hiyo.

“Niliona niiunge mkono serikali kwa kuchanja na baada ya kuchanja bado sijawa zombi na haiwezekani wataalamu wa afya wote wakawa na nia ya kuwaangamiza Watanzania,hivyo hatuna budi kuiunga serikali mkono kwenye vita hii ya kudhibiti maambukizi ya uviko-19 kwani muda wote iko kazini kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya njema,”alisema.

Naye Mjumbe wa Jumuiya hiyo, Askofu Richard Kamala,alisema nia ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Rais Samia, ni njema na inawatakia mema Watanzania,wale ambao wamechanja wawe kioo waisaidie serikali kuwaelimisha wengine waone umuhimu wa kuchanja.

“Chanjo ni hiari lakini baadaye kuna mambo mwili, inaweza kuwa lazima baada ya chanjo kwisha watu watatumia gharama zao, pia watakaotaka kusafiri kabla ya kuchanjwa watalazimika kuingia mfukoni (gharama zao) kuchanjwa,”alisema.

Askofu Kamala aliwataka wananchi ambao bado hawajachanjwa watumie kipindi hiki cha mlango wa rehema wakachanjwe kwa sababu chanjo ni salama,wajikinge na kuwakinga wengine na kuliweka taifa letu kwenye usalama zaidi.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa,Dk.Thomas Rutachunzibwa, hadi Septemba mwaka huu jumla ya watu 28,804 mkoani humu walikuwa wamechanjwa kati ya chanjo 90,000 zilizopokelewa.

Alisema lengo la nchi ni kuchanja asilimia 60 ya Watanzania wote na kuwataka wananchi kujitokeza kuchanja na kuepuka propaganda na uzushi kwani chanjo ni salama haina madhara.

Aidha alitoa rai kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kusaidia kufikisha elimu sahihi ya ubora na usalama wa chanjo kwa jamii ili kuwapa uelewa mpana kuhusu chanjo hiyo ya Uviko-19.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi,hadi sasa Watanzania milioni 1, wameshachanja kwa hiari huku serikali ikipokea chanjo nyingine ya Sinopharm kutoka nchini China,awali ilipokea chanjo ya Johnson & Johnson (JJ) kutoka Marekani

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news