RAIS SAMIA AKONGA NYOYO ZA WANANCHI MIGOGORO YA MATUMIZI YA ARDHI KATIKA VIJIJI

Na Munir Shemweta, WANMM Singida

Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuitaka timu ya Mawaziri nane inayotembelea mikoa kumi kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kufanya maamuzi bila kuleta taharuki na kwa maslahi mapana ya Taifa umeleta furaha kwa wananchi na viongozi kwenye maeneo ya vijiji hivyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa vijiji vitano vya Masimba, Mseko, Kizonzo, Nselembwe na Wembere vilivyopo kwenye Bonde Oevu la Wembele katika halmadhauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida wakati wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya hifadhi.

Timu ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta ikioongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi iko katika ziara ya mikoa kumi kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maamuzi ya migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 920 kati ya 975 ambavyo migogoro yake inashughulikiwa.

“Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kufanya maamuzi kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi bila kuleta taharuki kwa wananchi na kwa maslahi mapana ya Taifa” alisema Lukuvi wakati wa mikutano na wananchi.

Katika mkoa wa Singida timu ya Mawaziri pamoja na wataalamu kutoka wizara za kisekta ilitembelea baadhi ya maeneo ya vijiji 12 vya mkoa mwishoni mwa wiki kujionea hali halisi ya maeneo yenye mgogoro kwa lengo la kujiridhisha na maamuzi yaliyopendekezwa.
Sehemu ya wananchi wakishangilia uamuzi wa serikali kuwabakisha katika maeneo yao kwenye Bonde Oevu la Wembele katika halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida wakati wa ziara ya Mawaziri wa Kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya hifadhi.

Moja ya sehemu waliyotembelea ni kijiji cha Nduamughanga chenye vitongoji vya Mkulu, Nkungi na Majengo Mapya kwenye kata ya Mughunga wilaya ya Singida na kubaini sehemu ya vitongoji hivyo yenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 9.645 kuingia ndani ya mipaka ya Pori la Akiba Swagaswaga.

Eneo hilo lina kaya 269 zilizoanzishwa kimakosa kutokana na utata wa tafsiri ya mpaka wa wilaya ya Chemba na Singida unaopingana na GN ya hifadhi inayoonesha kuwa hifadhi ipo mkoa wa Dodoma pekee.

“Napenda niwaeleze kuwa, Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameamua mbaki kwenye maeneo yenu na eneo hili litafanyiwa tathmini na kuwekewa mpango wa matumizi bora ya ardhi pamoja na elimu ya uhifadhi kuendelea kutolewa kwa wananchi ili kujenga ufahamu wa hifadhi”. Alisema Waziri Lukuvi

Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda alipongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuamuru wananchi wanaoishi vijiji vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi kubaki maeneo yao na kuelezea uamuzi huo kuwa utaondoa hofu na taharuki waliyokuwa nayo wananchi kabla ya uamuzi wa serikali.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akizungumza katika kikao na wananchi wa vijiji vya Masimba, Mseko, Kizonzo, Nselembwe na Wembere vilivyopo kwenye Bonde Oevu la Wembele katika halmashauri ya wilaya ya Iramba wakati wa ziara ya Mawaziri wa Kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya hifadhi.

Mkoa wa Singida una vijiji vyenye migogoro ya mipaka na hifadhi ambapo katika utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri iliamuliwa vijiji hivyo vibaki na mipaka yake irejewe kwa njia shirikishi.

Vijiji hivyo ni Mlandala na Msosa vilivyopo wilaya ya Ikungi pamoja na vijiji vya Masimba, Mseko, Kizonzo, Nselembwe na Wembere vilivyopo katika halmadhauri ya wilaya ya Iramba.

Eneo la vijiji hivyo ni ardhi oevu yenye vitalu vya uwindaji wa kitalii ambapo Wananchi kutoka mikoa ya Singida, Shinyanga pamoja na Tabora wamevamia ardhi oevu ya Wembele kwa ajili ya malisho na kilimo katika eneo hilo chepechepe la bonde la wembele.

Bonde la Wembele ni chanzo cha maji ya mto Wembele na mtiririko wa maji ya ziwa Eyasi na Kitangiri. Eneo hilo ni muhimu kwa ajili ya mapito na mazalia ya wanayamapori na makazi ya ndege hai ambao wako hatarini kutoweka duniani.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi mkoani Singida wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya hifadhi.

Imeelekezwa katika vijiji hivyo tathmini itafanyika ili kutambua mipaka ya ardhi oevu kwa njia shirikishi na kuwekewa alama za kudumu. Aidha eneo lipandishwe hadhi kuwa hifadhi ya Ardhioevu Wembere Wetland Game Reserve na mipango ya matumizi ya ardhi iandaliwe.

Baadhi ya wananchi wakiwemo wabunge wameelezea uamuzi wa Rais kama njia ya kuleta suluhu ya migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya vijiji ambayo wananchi wake wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi bila kujua hatma yao.

Mmoja wa wananchi anayeishi kwenye jamii ya wafugaji aliyejitambulisha kwa jina la Iddy Selemani alisema, kwa sasa ana uhakika maeneo yao yatapangwa upya na kubainisha maeneo ya wafugaji na wakulima na hivyo kutoa muafaka wa matumizi ya ardhi katika maeneo yao.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mlandala wakiwasikiliza Mawaziri wa Kisekta wakati wa ziara ya Mawaziri wa Kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya hifadhi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kondoa mkoa wa Dodoma Mohamed Huseni Kova alipokea uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwabakisha ama kumega sehemu ya maeneo ya hifadhi kwa ajili ya wananchi kwa furaha na kuuelezea kuwa ni uamuzi mzuri uliolenga kuwaonea huruma wakulima na wafugaji.

” Ongezeko la watu linafanya kuwe na uhitaji mkubwa wa ardhi na uamuzi wa kuwabakisha wananchi unatoa huruma kwa kuwa kulikuwa na vijana wa maliasili waliotoa adhabu kali kwa wananchi walioingia maeneo ya hifadhi” alisema Kova.

Mawaziri wa wizara za Kisekta zinazojumuisha Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Ardhi, Maji, Mifugo na Uvuvi, Ulinzi pamoja na Maliasili na Utalii wanaendelea na ziara tarehe 11 Oktoba 2021 katika mkoa wa Tabora baada ya kuhitimisha mikoa ya Dodoma, Manyara na Singida ambapo watapeleka mrejesho katika vijiji vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi katika mkoa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news